Wakristo Gaza waomba amani huku mashambulizi ya Israeli yakiendelea

Mauaji ya kimbari ya Israeli huko Gaza, yaingia siku yake ya 446, yamesababisha vifo vya Wapalestina 45,338 na wengine 107,764 kujeruhiwa. Nchini Lebanon, Israel imewauwa watu 4,048 tangu Oktoba na kuendelea kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano,

By Mustafa Abdulkadir
Vita vya Israel dhidi ya Gaza vimefifisha sherehe za Krismasi. Picha: AFP / Others

Mji wa Ukingo wa Magharibi wa Bethlehem unajiandaa kusherehekea Krismasi bila maonyesho yake ya kitamaduni kwa mwaka wa pili mfululizo kutokana na vita vikali vya Israeli dhidi ya Gaza.

Jiji hilo, ikiumuisha Kanisa la Nativity, linaloaminika kujengwa kwenye sehemu takatifu ambapo Yesu Kristo alizaliwa, kwa sasa halina mazingira yoyote ya sherehe.

Badala yake, maombi na wito wa kukomesha vita vya Israeli dhidi ya Gaza vimechukua nafasi ya sherehe za kawaida.

Kwa kawaida, wakati huu wa mwaka, taa, vichochoro, na makanisa ya Bethlehemu hupambwa kwa mapambo ya Krismasi, huku mmoja wapo wa miti mizuri zaidi ulimwenguni ya Krismasi ukisimamishwa katika uwanja wa Manger karibu na kanisa maarufu. Jiji pia huwa na zogo na watalii wakati wa msimu wa likizo.

Lakini kwa mwaka wa pili, vita vya Israeli dhidi ya Gaza vimefifisha sherehe za Krismasi katika mji huo na kuwaibia wakaazi wake furaha hiyo. Sherehe za Krismasi za mwaka huu zimesalia kuwa ibada na ziara za familia.