Mzozo wa Mashariki ya Kati unaigharimu Kenya zaidi ya dola milioni 2 kila wiki

Uuzaji wa bidhaa nje unaathiriwa sana kwani wanunuzi wakuu katika Mashariki ya Kati bado hawapatikani kwa urahisi tangu Marekani na Israeli kuishambulia Iran Februari 28, 2026.

By
Wanunuzi wakubwa wa nyama kutoka kenya ni nchi za Mashariki ya kati / Reuters

Serikali ya Kenya inasema mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati unaigharimu nchi hiyo mamilioni ya pesa.

Uuzaji wa bidhaa nje unaathiriwa sana kwani wanunuzi wakuu katika Mashariki ya Kati bado hawapatikani kwa urahisi tangu Marekani na Israeli kuishambulia Iran Februari 28, 2026.

Mashambulizi ya kulipiza kisasi yalifuata.

Nchi nyingi za eneo la Ghuba zimefunga anga zao huku mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yakiripotiwa kuendelea.

"Tunatuma nyama yenye thamani ya zaidi ya $2.3milioni (Sh300 milioni) na bidhaa za wanyama Mashariki ya Kati kila wiki," Katibu wa Baraza la Mawaziri la Kilimo Mutahi Kagwe alisema.

Wanunuzi wakuu wa bidhaa za nyama nchini Kenya ni nchi za Mashariki ya Kati, haswa Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain, na Kuwait.

Saudi Arabia ndiyo mshirika mkubwa zaidi, ikiagiza nyama yenye thamani ya dola milioni 6.37 mwaka 2024.

"Hilo ni jambo ambalo tunapaswa kufikiria hasa pia bidhaa za chakula ambazo tumekuwa tukiiuzia Iran, ambayo pia imeathiriwa," anaongeza.

Bidhaa kuu ambazo Kenya inauza kwa Iran ni chai, kondoo na nyama ya mbuzi  na kahawa, huku bidhaa kuu za Iran zinazouzwa nje ya Kenya ni pamoja na  tambi, na petroli ambayo hutumika kwa mchanganyiko wa lami.

Waziri wa Kilimo wa Kenya anasema nchi inatafuta masoko mbadala ya bidhaa.

Pia iliyoathiriwa ni mauzo ya nje ya chai, hasa yanayouzwa kupitia Kituo cha Bidhaa cha Dubai Multi Commodities (DMCC) ambacho ndicho kituo kikuu cha biashara cha ukanda huria na bidhaa duniani.

"Kama unavyojua pia tuna sehemu yetu ya mauzo ya chai huko Dubai, DMCC ambapo ndiko tunakochanganya baadhi ya chai zetu hasa kwa ajili ya mauzo kwa baadhi ya nchi za Mashariki ya Kati," Kagwe aliongeza.

Serikali inasema Wizara yake ya Mambo ya Nje inafanya kazi ya kutathmini hali ya Mashariki ya kati na baadaye kushauri Wizara husika kuhusu hatua za kuchukua ili kulinda uzalishaji pamoja. Pia amesema hiyo itasaidia kuepusha uchumi kudhoofika dhidi ya athari zinazoweza kuepukika.