Kutana na Carter, Sokwe Mtu maarufu ndani ya hifadhi ya Mahale nchini Tanzania
Muda mwingi, Carter huonekana akitembea kwa utulivu ndani ya kundi kubwa la sokwe, akifurahia maisha ya amani anayoyaishi na jamii ya kundi lake.
Akichezacheza sokwe wengine, Carter anashindwa kuficha uchangamfu wake, anapokuwepo ndani na hifadhi ya milima ya Mahale, iliyopo mkoani Kigoma.
Akiwa na umri wa miaka 40, Carter ni mtoto kwa sokwe jike maarufu kwa jina la Calliope, aliyefariki mwaka 2009 akiwa na miaka 51.
Carter alikuwa na ndugu zaje wawili, wa kiume mmoja; aitwaye Cadmas, ambaye alikufa mwaka 2010 akiwa na miaka 18 baada ya kushambuliwa na aliyekuwa kiongozi wa kundi wakati huo (Alpha Male) aitwaye Pimu, na ndugu yake jike, Carmen.
“Kwa sasa, umri wake mkubwa unamfanya sokwe Carter kuonekana kama babu mlezi, mtulivu, mwema, mwenye kupenda kukaa karibu zaidi na sokwe wadogo kuliko madume wenye nguvu wanaoongoza kundi lake la Sokwe wa Mahale,” anasema Philipo Hassan, askari uhifadhi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Muda mwingi, Carter huonekana akitembea kwa utulivu ndani ya kundi kubwa la sokwe, akifurahia maisha ya amani anayoyaishi na jamii ya kundi lake.
Na nyakati zingine hupendelea kupata utulivu wa kujitenga na vurugu ambazo husababishwa na madume wa kundi lake.
“Pia hupenda kukaa na watoto, kuwatazama, na kucheza nao huku akitengeneza uhusiano wa kipekee unaowafanya watoto kumpenda na kumfuata kila mara,” anaeleza Philipo kutoka TANAPA.
Ikolojia inaonesha kuwa, madume wengi wa Sokwe, wenye umri wa kati ya miaka 20 na 30 huepuka sana kucheza na sokwe wadogo, wakihofia ‘kupotezewa heshima’ na ‘watoto hao’, katika jamii ya koo zao.
Uongozi katika ukoo wake
Ingawa ni dume aliyewahi kufika nafasi ya tano katika uongozi wa ukoo wake, Carter hajawahi kufika uongozi wa juu. Tangu akiwa kijana, Carter hajawahi vurugu za aina yoyote.
“Hapendi vurugu wala ugomvi na ndio maana hadi hii leo, hana majeraha makubwa kwenye mwili wake,” Philipo anasema.
Kitu pekee unachoweza kuona kwa Carter ni makovu ya michubuko michache tu ambayo aliipata akiwa na umri wa miaka 30 katika jitihada zake za kupambania sokwe jike wakiwa katika kipindi cha kupandwa.
Tabia yake kijamii
Nyakati pekee ambazo Carter huonesha msimamo mkali ni pale anapozungukwa na kundi la majike watupu, ambapo hutoa ishara ya kuunguruma kama utambulisho wa uwezo wake, bila kuanzisha vita wala kumuumiza yeyote na baadae hutulia akiona dume mwingine amesogea eneo alipo.
Hali hiyo humsaidia sana kuweza kupata majike pindi yanapokuwa kwenye joto. Dume hufanya vurugu kwa majike wakiwa katika hali ya kawaida jambo ambalo humsaidia kufanikisha kuwapata majike kirahisi wakiwa kwenye hali ya joto.
Sokwe mzee
Kwa sasa, Carter ndiye sokwe dume mwenye umri mkubwa kuliko madume wote walioko kundi la Sokwe wa Mahale.
Sokwe hufikia umri wa miaka 50 hadi 55 wakiwa mazingira yao asilia (msituni) na umri wa zaidi ya miaka 60 wakiwa maeneo ya bustani za wanyama.
Sokwe mwenye umri mkubwa kuliko wote duniani ni sokwe aitwaye Joao mwenye umri wa miaka 81, na anapatikana katika bustani ya Sokwe “Chimp Eden” iliyopo nchini Afrika Kusini.
Sokwe wa Mahale ni hazina ya utalii ambayo inaleta mapato kwa Taifa, inaimarisha uchumi wa jamii zinazozunguka hifadhi na kuongeza ajira kwa Watanzania.