Watu zaidi ya 5,000 wameondolewa katika makazi yao katika vijiji 10 vya jimbo la Sudan la Darfur Magharibi huku kukiwa na ukosefu wa usalama na mapigano kati ya jeshi na wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF), Shirika la Kimataifa kuhusu Uhamiaji (IOM) limesema.
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa, katika taarifa iliotolewa siku ya Jumapili, linasema mfumo wake unakisia kuwa watu 5,135 wamekimbia katika vijiji vya Darfur Magharibi vya eneo la Sirba kufikia Agosti 8 kufuatia kuzuka kwa mapigano katika sehemu ya Bir Saliba.
Wengi wa wale walioondolewa wako upande wa pili nchini Chad, shirika hilo lilisema.
Siku ya Jumamosi, Gavana wa Darfur Minni Arko Minnawi alisema jeshi la Sudan limetibua shambulio kubwa la RSF eneo la Bir Saliba.
Mji wa kimkakati
Bir Saliba uko kaskazini mwa El Geneina, mji mkuu wa Darfur Magharibi, na unachukuliwa kuwa muhimu kwa sababu ya sehemu uliopo katika njia zinazoelekea mjini. Kumekuwa na mapigano katika eneo hilo mara kwa mara kati ya RSF na jeshi pamoja na vikosi vyake washirika.
Mapigano kati ya jeshi la Sudan na RSF yamekuwepo tangu Aprili 15, 2023, kufuatia kutofautiana kuhusu ujumuishaji ndani ya jeshi. Vita hivyo vimesababisha vifo vya maelfu ya watu na kuondoa mamilioni katika makazi yao.
Kufikia mwishoni mwa mwezi Juni 2026, IOM ilikuwa imerekodi watu karibu milioni 8.69 walioondolewa katika makazi yao nchini Sudan, pamoja na wengine zaidi ya milioni 4.64, ambao walirudi katika maeneo yao ndani ya nchi au waliotoka nje ya nchi.
















