Waziri Mkuu wa Tanzania Mwigulu Nchemba, amesema serikali ya nchi hiyo inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha Uwanja wa Ndege wa Mwanza unaboreshwa na kujengwa katika hadhi ya kimataifa ili kuendana na hadhi ya jiji hilo akama kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi Kanda ya Ziwa.
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma Mei 13, 2026, Waziri Mkuu huyo amesema kuwa serikali ya nchi hiyo inatambua umuhimu wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza na imeendelea kufanya jitihada mbalimbali kuhakikisha unakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa pamoja na kukidhi viwango vya kimataifa.
“Zipo jitihada ambazo zimekuwa zikifanyika kuhakikisha kwamba uwanja wa ndege wa Mwanza unaendana na hadhi ya Mwanza kama kitovu cha shughuli za kiuchumi Kanda ya Ziwa,” alisema Nchemba.
Aidha, kiongozi huyo ameongeza kuwa nchi hiyo inaendelea na mazungumzo ya kuongeza eneo la uwanja huo ili kuwezesha upanuzi wa njia ya kurukia ndege (runway) pamoja na maboresho mengine muhimu ya miundombinu.
Katika hatua nyingine, Nchemba amesema kuwa serikali ya nchi hiyo imekubaliana kujenga jengo jipya la abiria litakalokuwa na hadhi ya kimataifa na kuendana na mahitaji ya muda mrefu ya uwanja huo.
“Imekuja kukubalika kwamba tujenge jengo ambalo halitahitaji kubomolewa tena baada ya muda mfupi, bali jengo lenye hadhi na viwango vya viwanja vya ndege vya kimataifa,” aliongeza.















