Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, amewataka wafanyakazi wa nchi hiyo kuwa chachu ya uzalishaji, ufanisi na nidhamu kazini.
Akizungumza mkoani Njombe, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, kiongozi huyo alisema kuwa serikali yake itaendelea kusikiliza hoja za wafanyakazi kwa utaratibu, kwa kuzingatia uwezo wa uchumi, sheria za nchi na maslahi mapana ya taifa hilo.
Pia, alisisitiza kuwa serikali yake itaendelea kuweka mkazo katika kukuza ujuzi, hususan kwa vijana, ili kuwaandaa Watanzania kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kisiasa unaohitaji maarifa, teknolojia na ubunifu.
“Dhamira ya serikali ni kuona kila mfanyakazi anafanya kazi katika mazingira salama, yenye heshima, haki na yanayomwezesha kuchangia kikamilifu katika ujenzi wa taifa,” alisema Rais Samia.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Kanda ya Afrika Mashariki, Caroline Mugala, ameipongeza Tanzania kwa kuimarisha ajenda ya kazi zenye staha, haki za kijamii na majadiliano ya wadau wa utatu katika sekta ya kazi.
Mei Mosi ya kila Mwaka, Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani.
Lengo ni kuhamasisha utoaji wa haki msingi kwa wafanyakazi, kuboresha masharti ya kazi ili kuongeza tija na ufanisi zaidi sanjari na kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wafanyakazi wengi.









