Kwa nini mafuriko yanatokea katika miji mikuu?

Miji mikuu mingi ilitengwa na mamlaka za kikoloni kwa kuzingatia upatikanaji wa bandari za baharini au maeneo ya kimkakati ya usambazaji na usafirishaji wa bidhaa zao.

By Coletta Wanjohi
Mafuriko katika jiji la Nairobi baada ya mvua kubwa kunyesha 6 Machi 2026 / AP

Jiji kuu la Nairobi nchini Kenya, lilikumbwa na mafuriko makubwa katika maeneo mbalimbali mbali baada ya mvua kubwa iliyonyesha kuazia usiku ya 6 Machi 2026.

Mpaka sasa, idadi ya vifo inayotokana na mafuriko hayo imeongezeka kufikia 42.

Mbali na Nairobi, mikoa mengine kadhaa pia imeshuhudia mafuriko.

Hii ni kulingana na taarifa ya polisi.

Mamlaka nchini humo imesema, vifo 26 kati ya hivyo vimetokea Nairobi, ambapo athari kubwa imeonekana katika maeneo tambarare na makazi yasiyo rasmi, ambapo nyumba kadhaa zilifunikwa na maji, huku magari yakielea.

Uharibifu mkubwa ulishuhudiwa pia katika biashara na miundombinu ya mji na mikoa mengine.

Huku timu za uokoaji zikiendelea kuwahamisha wakazi kutoka maeneo yaliyofurika.

Hali hii haikushuhudiwa Nairobi pekee, mji mkuu wa Uganda, Kampala pia ulikumbwa na mafuriko yaliyoathiri usafiri, biashara, na watembea kwa miguu katika maeneo mbalimbali ya jiji.

Hali hii pia ilisababisha msongamano mkubwa wa magari.

Lakini kwa nini hasa miji mikuu hufurika?

Kwa kuanzia, miji mikuu mingi ilitengwa na mamlaka za kikoloni kwa kuzingatia upatikanaji wa bandari za baharini au maeneo ya kimkakati ya usambazaji na usafirishaji wa bidhaa zao.

Miongo kadhaa baadaye, baada ya uhuru miji hii iliongezewa majukumu mengine ya utawala bila kufanyiwa uboreshaji mkubwa wa miundombinu yenye kukidhi ongezeko la mahitaji. Hivyo, baadhi yao kushindwa kustahimili mtiririko mpya wa idadi ya watu na shughuli za kila siku.

Tatizo kubwa linaanzia katika miundombinu ya maji taka na mifereji ya maji ambayo haiwezi kudhibiti mtiririko wa juu. Kwa hivyo mvua inaponyesha, maji hukosa sehemu ya kwenda hivyo kusababisha mafuriko.

Ukuaji wa miji umechukua sehemu ya ardhi na mimea hivyo kuzuia maji kuingia ardhini.

Pia kuna sababu za asili ambapo mvua nyingi hulemea mifumo iliyoundwa kwa hali mbaya sana.

Katika miji mingi, ujenzi unafanywa kwenye maeneo tambarare, ardhi oevu, na hivyo kuziba njia za asili za maji ambazo huzuia mifereji ya asili ya maji kupita kwa kasi.

Miji iliyo katika maeneo ya tambarare au pwani huathirika na mafuriko kutoka kwa mito au mawimbi ya dhoruba.

Hii kwa mfano ni kesi ya Mahe mji mkuu wa Shelisheli, Antananarivo ya Madagascar.

Kama mwathiriwa wa hivi punde wa mafuriko, Nairobi inapojitahidi kurekebisha hasara ya mafuriko ya mwishoni mwa juma  wananchi wana wasiwasi kwamba ikiwa mifumo ya mifereji ya maji haitarekebishwa miongoni mwa hatua nyengine muhimu, litakuwa janga jengine linalosubiri kutokea tena.