Kenya yapiga marufuku raia wake kujiorodhesha katika Jeshi la Urusi

Mawaziri wa mambo ya nje wa Kenya na Urusi walikutana mjini Moscow na kukubaliana kuwarudisha nyumbani wale ambao tayari wamejiandikisha kuipigania Urusi nchini Ukraine iwapo watakuwa tayari.

By
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Lavrov na wa Kenya Musalia Mudavadi walikutana Moscow / Reuters

Kenya ilisema Jumatatu kwamba imekubaliana na Urusi kutowaruhusu raia wa Kenya kujiandikisha katika jeshi la Urusi ili kushiriki katika vita dhidi ya Ukraine. Hatua hii imekuja baada ya idadi kubwa ya waliojiandilisha kuibua hasira katika baadhi ya nchi za Afrika.

Kenya inasema kuwa zaidi ya Wakenya 1,000 wameajiriwa kupigana, wakivutiwa na mishahara ya kila mwezi ya dola elfu kadhaa na marupurupu ya zaidi ya $6,000 kwa wanajeshi wa kulipwa.

Baada ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov mjini Moscow, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi alisifu uhusiano huo na Urusi, ikiwa ni pamoja na utambuzi wa Usovieti na uhuru wa Kenya kutoka kwa Uingereza mnamo 1963.

Kuhusu suala la Wakenya kupigana katika kile Urusi inachokiita "operesheni maalum ya kijeshi" nchini Ukraine, Mudavadi alisema makubaliano yamefikiwa kutoruhusu tena Wakenya kujiandikisha kupigana.

"Waziri amezungumza nasi kuhusu suala la ustawi wa Wakenya walioko Urusi na haswa wale wanaohusika katika operesheni hiyo maalum," Mudavadi alisema katika kikao cha habari cha pamoja na Lavrov.

"Na ninataka kueleza wazi kwamba sasa tumekubaliana kwamba Wakenya hawataandikishwa kupitia Wizara ya Ulinzi (ya Urusi) - hawatastahiki tena kuorodheshwa," alisema.

"Hakutakuwa na uandikishaji zaidi."

Aliongeza kuwa huduma za kibalozi zitaandaliwa kupitia njia muafaka za kidiplomasia kwa Wakenya ambao tayari wamejiandikisha na kuhitaji usaidizi.

Lavrov alisema kuwa raia wa Kenya walisaini makubaliano kwa hiari ya kupigana pamoja na jeshi la Urusi.

Haijulikani ni Waafrika wangapi wameenda kupigana nchini Ukraine, lakini Ukraine inasema zaidi ya Waafrika 1,700 wanapigana upande wa Urusi. Wizara ya Ulinzi ya Urusi haikujibu ombi la maoni.

Ripoti ya kijasusi ya Kenya iliyowasilishwa kwa wabunge mwezi Februari ilisema kuwa zaidi ya Wakenya 1,000 wameajiriwa kupigana upande wa Urusi katika vita vya Ukraine, mara tano zaidi ya ilivyokadiriwa hapo awali.

Wanasiasa wa Kenya wameelezea kile wanachosema ni mtandao wa maafisa wa serikali walaghai ambao wameshirikiana na makundi ya magendo ya binadamu kuwaajiri Wakenya kupigania Urusi nchini Ukraine.

Mudavadi alisema Kenya na Urusi zinaweza kuimarisha ushirikiano katika masuala ya nishati, utalii na kilimo.

Uhusiano kati ya Kenya na Urusi ni mpana zaidi kuliko huo."