Kiongozi wa upinzani Uganda Bobi Wine atoroka nchini baada ya uchaguzi uliokuwa na mvutano

Kiongozi wa upinzani Bobi Wine anathibitisha kuwa ametoroka nchini Uganda, lakini hakufichua alipokwenda, baada ya kujificha kwa muda kwa kuhofia maisha yake.

By
Rais Yoweri Museveni wa Ugandan alishinda kwa asilimia 71.6 ya kura, kwa mujibu wa matokeo ambayo Wine ameyakataa. / AP

Kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine amesema Jumamosi kwamba ameikimbia nchi kuepuka msako wa jeshi baada ya Uchaguzi wa urais wa nchi hiyo.

Wine, ambae jina lake halisi ni Kyagulanyi Ssentamu, alikuwa mafichoni muda mfupi tu baada ya Uchaguzi wa Januari 15.

Rais Yoweri Museveni wa Ugandan alishinda kwa asilimia 71.6 ya kura, kwa mujibu wa matokeo ambayo Wine ameyakataa.

Kwa wiki kadhaa, sehemu aliyokuwa amejificha Bobi Wine haijulikana, huku kukiwa na wasiwasi kuhusu usalama wake baada ya Mkuu wa Majeshi, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, mara kadhaa kutoa vitisho dhidi yake kupitia mtandao wa X.

Kainerugaba, mtoto wa Rais, alisema Wine anatafutwa kwa makosa ambayo hayakutajwa. Polisi nchini Uganda inasema haimtafuti.

Katika ujumbe wa video iliyowekwa katika mtandao wa X Jumamosi, Wine alisema kuwa amefanikiwa kuondoka Uganda lakini hakutaja sehemu alipo.

“Waganda wenzangu na marafiki zangu wa Uganda duniani kote, mpaka muda huu mnapoona video hii, itakuwa nimeondoka Uganda kwa majukumu muhimu nje ya Uganda,” amesema.

‘Nitarudi’

“Na kwa muda sahihi nitarudi na kuendelea na mapambano. Nawashukuru nyote Waganda wenzangu walionificha na kunilinda muda wote huo wakati utawala ulipokuwa unanitafuta."

Amesema isingewezekana kwa vikosi vya Uganda kumpata "kwa sababu watu walinilinda."

Wanajeshi wa Uganda walivamia nyumba ya Wine siku moja baada ya Uchaguzi wa Januari 15, lakini kiongozi huyo wa upinzani alikuwa tayari ameshaondoka, akihofia maisha yake baada ya wiki kadhaa za kampeni akiwa amevaa 'helmet' katika mikutano ambayo mara nyingi ilihudhuriwa na vikosi vya ulinzi.

Wine, mgombea maarufu katika wagombea saba waliosimama dhidi ya Museveni, alivutia zaidi vijana maeneo ya mijini.

Mwezi Mei, Museveni mwenye umri wa miaka 81 ataapishwa kwa muhula wa saba ambao utamfanya aendelee kuwa madarakani kwa karibu miongo mitano.

Wafuasi wake wanamsifu kwa kuleta amani na utulivu ambapo Uganda imekuwa makazi ya maelfu ya wakimbizi kutoka nyengine za Afrika. Lakini viongozi wa upinzani, wakiwemo baadhi waliokuwa washirika wake wa karibu, wanamlaumu kwa kile wanachokiona kama ukandamizaji wa demokrasia.