Shamba la mihogo ambalo wakati mmoja lilikuwa likiwapa chakula watoto watano wa Marie Kavira sasa hivi hakuna kitu, limekuwa sehemu kavu.
Mjane huyo mwenye umri wa miaka 34 alikuwa akishughulikia shamba hilo, lakini akalazimika kukimbia wakati waliposhambuliwa usiku wa mwezi Oktoba mwaka uliopita katika kijiji cha Ituri eneo la Djugu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
“Tulikimbia tu tukiwa na nguo zetu za kulala,” Kavira ameiambia TRT Afrika. Sasa hivi anaishi katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya nchi viungani vya Bunia. “Nilikuwa na mbegu kwa ajili ya msimu ujao. Nilikuwa nimeziweka kwenye kiroba karibu na majifya ya kupikia. Sikuwa na muda.”
Mashariki ya DRC ukikosa msimu mmoja wa kupanda, familia inakosa chakula kwa miezi sita. Ukikosa misimu miwili, na utapiamlo unakuwa sehemu ya maisha yenu.
Sasa Kavira amekosa misimu mitatu ya kulima.
Hayuko peke yake. Kulingana na tahadhari iliotolewa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), raia wa DRC zaidi ya milioni 26.5 —karibu mtu mmoja kati ya wanne—wanashindwa kupata chakula. Miongoni mwao, watu zaidi ya milioni 3.6 wako katika hali ya dharura, kiwango ambacho ni kimoja tu juu ya ukame.
Mahesabu ya mama
Katika mikoa ya mashariki ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Ituri, na Tanganyika, mapigano yamekuwa yakifanyika kila wakati, familia kuondoshwa katika makazi yao, mashamba kuchomwa moto, na watu wanakuwa wanakabiliwa na njaa kali.
Mtoto mdogo wa Kavira, ni wa kiume ana umri wa miaka miwili na jina lake ni Baraka. Pamoja na jina kuwa na maana muhimu, lakini umbo la mtoto huyo linaeleza maana tofauti. Mikoni yake ni membamba. Na nywele zake zimekuwa nyekundu —ishara ya kukosa lishe ya protini. Macho yake yanang’ong’wa na wadudu.
Baraka ni miongoni mwa watoto milioni 4.18 walio chini ya umri wa miaka mitano kote DRC ambao wanahitaji kutibiwa kutokana na utapiamlo. Zaidi ya milioni 1.3 miongoni mwao, ikiwemo Baraka, wana utapiamlo mbaya - hali ambayo inaweza kusababisha kifo katika kipindi cha wiki kadhaa kama hawatotibiwa.
Tangu Januari 2026, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani limekuwa na mradi wa dharura wa chakula na fedha ambao umewafikia watu karibu milioni 1.3 katika maeneo yaliyoathirika zaidi mikoa ya mashariki. Idadi hiyo inaonekana kubwa ila mpaka ujuwe uzito wa tatizo lilivyo: Watu milioni 26.5 wanakabiliwa na njaa kali au hata zaidi.
Lakini kurudisha hali kama ilivyo, mashariki mwa DRC, inaonekana kama neno la kigeni. Mapigano yanayosababisha hali hii hayaonekani kumalizika.
Tukirudi Bunia, Marie Kavira bado hajakata tamaa. Amesikia kuhusu ugavi wa mbegu, hafla ilioandaliwa na mshirika wa eneo wa FAO. Alitembea kwa saa tatu kujisajili. Atatembea tena kwa saa tatu. Akipata mbegu - atatafuta shamba ndogo karibu na kambi yao afanye kilimo.
“Natama mihogo sana,” anasema. “Nawaza namna nitakavyotoa muhogo ardhini, niuoshe, niuchome, na niwape watoto wale hadi wasema ‘Mama, nimeshiba.’ Unajuwa ni muda gani tangu niskie maneno hayo?”
Alimuangalia Baraka, ambaye alikuwa amelala kifuani mwake. Anapumua pole pole sana. Mbavu zake zinaonekana hafifu.
“Nitapanda chochote watakachonipa,” alisema. “Nitalinda kwa nguvu zote. Na kama wanajeshi watakuja tena, nitakimbia na mbegu mkononi mwangu. Madamu nitakuwa na mbegu, basi nitakuwa na sababu ya kuendelea kuishi.”















