Jeshi la Uganda limekanusha madai ya kuwashikilia wanaharakati wawili wa Kenya Bob Njagi na Nicholas Oyoo, ambao walitekwa nyara mjini Kampala, Uganda, Oktoba 1.
Mawakili wawili wa Uganda walikuwa wamedai kuwa wawili hao walikuwa wanazuiliwa katika kambi ya jeshi huko Mbuya, Kampala.
Katika majibu yao kwa kesi iliyowasilishwa na mawakili wawili kwenye Mahakama Kuu ya Uganda, Jeshi la Uganda (UPDF) lilisema lilifanya uchunguzi na kupekua vituo vyote muhimu katika maeneo yao lakini hakuna taarifa kuhusu wanaharakati hao wawili waliotoweka.
Jeshi hilo lililotajwa kuwa mmoja wa waliohojiwa katika kesi hiyo, limekanusha kuhusika katika utekaji nyara kwa wanaharakati wa Kenya Bob Njagi na Nicholas Oyoo.
Uamuzi wa mahakama kuhusu suala hilo unatarajiwa kutolewa siku ya leo Alhamisi.
Silas Kamanda, Kanali wa UPDF ambaye ni mkurugenzi wa masuala ya kisheria jeshini, aliiambia mahakama kuwa jeshi la Uganda lilifanya uchunguzi na kupekua vituo vyote muhimu vya mahabusu, sajili za watu waliofungiwa, na rekodi za ulinzi, na hawakupata taarifa zozote kuhusu wanaharakati hao Nicholas Oyoo na Bob Njagi.
Kanusho hilo la kijeshi limekuja wiki mbili baada ya Jeshi la Polisi la Uganda, katika mkutano na waandishi wa habari, kukanusha taarifa za utekaji nyara na kusema kuwa bado hawajapata ripoti rasmi.
Hii inazua maswali kuhusu kile mamlaka ya Uganda inafanya kuhakikisha wawili hao wanapatikana baada ya kutekwa mchana. Oyoo na Njagi walikuwa wamesafiri hadi Uganda kumuunga mkono mgombea urais wa upinzani Bobi Wine.
Kwa muda wa wiki tatu, familia zao na mashirika ya haki za binadamu yamekuwa yakipaza sauti yakitaka waachiliwe, Serikali ya Kenya ilikuwa imewahakikishia familia kuwa Balozi wa Kenya nchini Uganda alikuwa anafuatilia suala hilo.
Siku ya Jumanne, Amnesty International, Chama cha Wanasheria wa Kenya, na Vocal Africa walizindua ombi la kimataifa kumtaka Rais wa Uganda Yoweri Museveni kuwaachilia wawili hao.
Mahakama Kuu ya Uganda inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu kesi ya hiyo siku ya Alhamisi.