Mkuu wa Ujasusi wa Uturuki (MIT), Ibrahim Kalin, amekutana na Mkuu wa Ujasusi wa Ugiriki (EYP), Themistoklis Demiris, mjini Athens wiki iliyopita, kwa mujibu wa taarifa kutoka vyanzo vya usalama.
Katika mkutano huo, Kalin na Demiris walijadili uhusiano wa mataifa hayo mawili pamoja na yanayojiri katika kanda, huku pande hizo mbili zikitathmini hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kushughulikia masuala yaliyopo, iliripoti TRT Haber.
Mazungumzo hayo yalisisitiza umuhimu mkubwa wa uhusiano kati ya Uturuki na Ugiriki katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Bahari ya Aegean na Mediterania ya Magharibi, usalama wa NATO, ushirikiano wa kijasusi, pamoja na juhudi za kukabiliana na ugaidi, uhalifu uliopangwa, uhamiaji harari na biashara haramu ya kusafirisha watu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mazungumzo hayo pia yaliangazia vita vya Marekani dhidi ya Iran, enzi mpya nchini Syria, umoja wa kisiasa wa Libya, vita vya Israel dhidi ya Gaza pamoja na ukiukaji unaoendelea na sera za Israel za kukalia maeneo katika Ukingo wa Magharibi . Aidha, pande hizo zilijadili mashambulizi ya Israel dhidi ya Syria na Lebanon.
Pande zote mbili zilikubaliana kuhusu umuhimu wa kudumisha na kuendeleza kasi iliyopatikana hivi karibuni katika mapambano dhidi ya ugaidi na makundi ya uhalifu uliopangwa, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano huo kufikia kiwango cha kimkakati.
Kalin wa MIT na Demiris wa EYP pia walikubaliana kuimarisha zaidi ushirikiano wa karibu kati ya mashirika hayo mawili ya kijasusi katika masuala ya nchi mbili na masuala ya kikanda.



























