Wafuasi 300 wa upinzani wamekamatwa wakati wa kampeni nchini Uganda
Vyombo vya usalama nchini Uganda vimewakamata wafuasi na maafisa zaidi ya 300 kutoka chama cha mgombea wa urais wa upinzani Bobi Wine tangu kampeni za uchaguzi wa Januari kuanza mwezi uliopita, alisema msemaji wa chama hicho Jumanne.
Nyota wa muziki aliyekuwa mwanasiasa, Bobi Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, anamkabili Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 81 kwa mara ya pili.
Aidha Bobi Wine ameshika nafasi ya pili katika uchaguzi uliopita mwaka 2021.
Sasa akiwa kiongozi wa nne Afrika aliyetawala kwa muda mrefu zaidi, serikali ya Museveni imebadilisha katiba mara mbili kuondoa kizuizi cha umri na muda wa kusalia madarakani, jambo lililomfanya kusalia madarakani tangu 1986.
Wafuasi wengi wamekamatwa wiki hii mjini Kampala, ambapo Wine alianza kampeni yake siku ya Jumatatu, alisema Joel Ssenyonyi, msemaji wa chama cha Bobi Wine, National Unity Platform (NUP), kwa shirika la Reuters.
"Zaidi ya watu 300 wamekamatwa tangu kampeni kuanza. Serikali hii iko na hofu, inatumia mfumo wa kukamata watu kama njia ya kuwaogopesha na kudhibiti wananchi wetu," alisema Ssenyonyi.
Wengi wa waliokamatwa ni wafuasi wa Bobi Wine, lakini pia wanajumuisha waandaji wa kampeni, wasaidizi wa Bobby Wine na maafisa wengine, alisema.
Msemaji wa polisi, Rusoke Kituuma, hakutoa ufafanuzi wowote.
Katika mkutano wa kampeni uliofanyika Jumatatu eneo la Kawempe mjini Kampala, vyombo vya usalama vilitumia mabomu ya kutoa machozi na mabomu ya maji kuwatawanya wafuasi wa Bobi Wine, kama ilivyoonyeshwa na video iliyorushwa na kituo cha televisheni cha NTV.
Video iliyopostiwa kwenye akaunti ya Wine kwenye mtandano wa X mwishoni mwa Jumatatu pia ilionyesha polisi wakitumia vipulizi vya pilipili kwa wafuasi wake. Mtu aliyevaa nguo za kawaida aliyejitokeza kando ya maafisa wa usalama alionekana akiwapiga wafuasi kwa fimbo.
Angalau watu 100 walikamatwa Jumatatu na wengine wengi walikamatwa Jumanne katika mkutano mwingine kwenye mipaka ya Kampala, alisema Ssenyonyi.
Polisi walisema katika taarifa mwishoni mwa Jumatatu kuwa walikamata watu saba baada ya migongano na wafuasi wa Bobi Wine, wakidai walirusha mawe na kujeruhi maafisa saba.
"Vyombo vya usalama vilijibu kwa kutumia mbinu za kudhibiti umati wa watu wenye vurugu," ilisema taarifa hiyo.
Bobi Wine anasema Museveni alishinda uchaguzi uliopita kwa njia za ujanja za kuingiza kura nyingi, kuaogopesha wapiga kura, rushwa na mbinu nyingine za udanganyifu.
Hata hivyo maafisa wa chama tawala wamekanusha madai hayo.