Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan ilitangaza siku ya Jumatatu kuwa imerudisha uanchama wake tena na kushiriki kamili katika IGAD, miaka miwili baada ya kusitisha uanachama wake.
Serikali ya Sudan iliamua kuhuisha tena nafasi yake katika IGAD, ikinukuu "taarifa chanya" kutoka kwa sekretarieti ya shirika hilo ambayo ilithibitisha kuheshimu mifumo ya msingi inayoongoza ushirikiano wa kikanda, wizara hiyo ilisema.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa "shirika liliahidi kutoingilia masuala ya ndani ya nchi wanachama, ikiwa ni pamoja na kutambua kikamilifu mamlaka ya Sudan, uhuru wa mipaka, umoja wa kitaifa na usalama wa taasisi zake za serikali zilizopo."
Sudan pia ilisema amani na usalama wa kimataifa vinasalia kuwa miongoni mwa "vipaumbele vyake vya juu" na kwamba inafanya kila juhudi kuvilinda katika ngazi za kikanda na kimataifa, na kuongeza kuwa inaona ushirikiano wa kikanda kama msingi wa ushirikiano mpana wa kimataifa.
Khartoum ilisitisha uanachama wake katika IGAD mnamo Januari 20, 2024, ikitaja kile ilichoeleza kuwa ni kuvuka mipaka kwa shirika hilo, ikiwa ni pamoja na kuweka hali ya Sudan kwenye ajenda ya mkutano wa 42 wa Umoja huo bila ya kuishauri nchi hiyo.
















