Kanali Kizza Besigye si jina geni kwenye ulingo wa siasa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Licha ya kukabiliwa na kesi ya uhaini, ambayo imemlazimu kuwepo ndani toka mwishoni mwa mwaka 2024, mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 70, ana historia na ukaribu wa kipekee na Rais Yoweri Museveni wa Uganda.
Je, unafahamu kuwa Besigye aliwahi kuwa daktari binafsi wa Rais Museveni?
Mara baada ya kuhitimu shahada yake ya utabibu kutoka Chuo Kikuu cha Makerere mwaka 1980, Besigye maarufu kama Ssenyondo (Nyundo kubwa), aliingia msituni na kuhuduma kama daktari binafsi wa Yoweri Museveni, ambaye alikuwa mpiganaji wa kikundi cha National Resistance Army, vilivyokuwa vikipambana na majeshi ya serikali ya Uganda, kati ya mwaka 1981 mpaka 1986.
Hata hivyo, kama wasemavyo Waswahili kuwa, kila chenye mwanzo, basi ni lazima kiwe na mwisho, na ndivyo ilivyotokea kwa Besigye na Museveni.
Ilipofika mwishoni mwa miaka ya 90, wawili hao walianza kutofautiana hadharani, huku Besigye akimtihumu na kumkosoa vikali aliyekuwa swahiba wake, kwa uongozi mbovu na wa kifisadi.
Besigye alimtuhumu Rais Museveni kwa kwenda kinyume na itikadi na sera za kidemokrasia, ambazo alikuwa akizipigania na kuzihubiri wakati wa vita vya msituni.
Miaka 11 baadae, Besigye aliamua kutupa karata yake na kugombea kiti cha Urais dhidi ya Museveni, licha ya kushindwa mfululizo kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2006, 2011, na 2016 mtawalia.
Amekuwa kiongozi wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC) kwa muda mrefu sasa na amemuoa Winnie Byanyima, mwanasiasa wa zamani wa nchi hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Ukimwi (UNAIDS).

















