Kiongozi Mkuu wa Iran Alireza Arafi
Kiongozi Mkuu mpya wa kidini nchini Iran ni Alireza Arafi, ni kiongozi muhimu wa kidini na kisiasa katika mfumo wa utawala wa nchi hiyo.
Hivi sasa ndie aliyeteuliwa kukaimu nafasi hiyo kufuatia kuuawa kwa Ali Khamenei.
Ana umri wa miaka 67 mzaliwa wa mji wa Meybod, katika mkoa wa Yazd amepata mafunzo ya muda mrefu katika taasisi za dini na urasimu za Iran.
Elimu yake alipata kutoka kwa wanazuoni wa dini maarufu na kupata cheo cha mujtahid, ambacho kinampa uwezo wa kutoa maamuzi kuhusu hukumu za Kiislamu.
Katiba ya Iran inaruhusu kuteuliwa kwa kiongozi wa muda kabla yule wa kudumu kuchaguliwa. Huyu anachaguliwa na Baraza linalojumuisha rais, mkuu wa mahakama, na mjumbe wa Baraza la Ushauri.
Baadaye kuna Bunge la viongozi 88 wa dini wanaochaguliwa baada ya kila miaka minane, ndiyo linakaa kumteua kiongozi mkuu wa nchi.
Mchakato huu hufanyika kwa njia ya siri na raia hawana nafasi ya kupiga kura ya moja kwa moja.
Huyu wa sasa Alireza Arafi atakaa kwenye wadhifa huo kwa muda, na tayari kuna viongozi kadhaa ambao wanapewa nafasi ya kumrithi Ali Khamenei akiwemo mtoto wake Mojtaba Khamenei mwenye umri wa miaka 56.
Mwingine ni Rais wa zamani Hassan Rouhani mwenye umri wa miaka 77 na mjukuu wa aliyekuwa Kiongozi Mkuu Khomeini, Hassan Khomeini ambaye ana umri wa miaka 53.
Kiongozi wa muda wa sasa Alireza Arafi alijiunga na Baraza la watu 12 lenye uwezo mkubwa wa Katiba 2019. Baraza hilo ndilo linawafanyia mchujo wagombea wa ubunge na nafasi zingine za kugombea kisiasa.