| Swahili
ULIMWENGU
1 dk kusoma
Rais wa China asema hatoipatia Iran silaha: Trump
“Alisema hatatoa vifaa vya kijeshi. Hio ni kauli muhimu sana", Rais Trump wa Marekani amesema baada ya kukutana na Rais Xi wa China, akiongeza kuwa China inataka kuona Mlango-Bahari wa Hormuz ukifunguliwa.
Rais wa China asema hatoipatia Iran silaha: Trump
Rais wa Marekani Trump amesema China inataka Mlango wa Hormuz uwe wazi. / / Reuters

Rais wa Marekani Donald Trump amedai kwamba Rais wa China Xi Jinping alimwambia kuwa China haitoipatia Iran vifaa vya kijeshi, na pia anaunga mkono kufunguliwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz.

Trump alisema hayo baada ya kukutana na Xi mjini Beijing, katika mahojiano na shirika la habari la FOX News.

“Alisema hatatoa vifaa vya kijeshi. Hio ni kauli muhimu sana", Trump alisema alipoulizwa kama walizungumzia kuhusu msaada wa China kwa Iran.

Trump pia aliongeza kuwa Xi alisema China inataka Mlango-Bahari wa Hormuz ubaki wazi, kwa sababu China hununua kiasi kikubwa cha mafuta kutoka eneo hilo.

“Alisema wananunua mafuta mengi huko, na wanataka kuendelea kufanya hivyo,” Trump alisema.

Aliongeza pia kuwa Xi angependa kuona makubaliano yakifikiwa kuhusu suala hilo, na alisema yuko tayari kusaidia inapowezekana.

Hata hivyo, mamlaka za China hazikutoa ufafanuzi wowote hadi sasa kuhusu madai ya Trump.

Taarifa rasmi ya China kuhusu mazungumzo hayo haikuzungumzia Iran wala Mlango-Bahari wa Hormuz. Ilisema tu kuwa viongozi hao wawili walijadili masuala muhimu ya kimataifa na kikanda, ikiwemo hali ya Mashariki ya Kati, mgogoro wa Ukraine, na rasi ya Korea.

CHANZO:Anadolu Agency