Burkina Faso yakanusha madai ya shirika la Haki za Binadamu kuhusu mauaji ya halaiki
Mamlaka ya Burkina Faso imesema mapambano dhidi ya ugaidi yanafanywa kwa kuzingatia sheria za kitaifa na ahadi za kimataifa kuhusu haki za binadamu.
Msemaji wa serikali ya Burkina Faso, Gilbert Ouédraogo, amekanusha madai ya ripoti iliyochapishwa Aprili 2, 2026, na Shirika la kutetea Haki za Binadamu (HRW) inayodai kuwepo kwa ukiukwaji wa haki za binadamu nchini humo.
Ripoti ya HRW ilidai kwamba serikali ya nchi hiyo na vikosi inavyoshirikiana navyo imeua idadi kubwa ya raia, hata kuliko idadi ya magaidi tangu serikali kuingia madarakani mwaka 2023.
Serikali ilieleza chapisho la HRW kuwa “ripoti bandia” na “yenye madai yasiyo na msingi, jambo ambalo HRW imezoea kufanya”, kulingana na Ouédraogo.
Aidha, serikali iliongeza kuwa haishangazwi na matendo ya shirika hili, ambalo “halina taarifa halisi kuhusu yanayotendeka wala hata kuwa na ofisi wala uwakilishi nchini Burkina Faso.”
‘Taarifa zisizo na msingi’
Ouédraogo pia alilaumu HRW kwa kusambaza mara kwa mara “madai kutoka kwa watu wanaolipwa, kwa kutoa taarifa zisizo na msingi.”
HRW haijatoa ufafanuzi wowete kuhusu maelezo ya serikali ya Burkina Faso.
Mamlaka ya Burkina Faso wanasema wanatambua “upungufu wa mbinu za HRW,” ambao, kwa maoni yao, unalenga “kuharibu jina la wafuasi wa taifa la Burkina Faso na vikosi vyetu vyenye ushujaa ili kuonekana huko nje kama wakiukaji wa haki za binadamu, kwa ajili ya kutimiza malengo mabaya ya ukoloni dhidi ya nchi yetu.”
Serikali iliongeza kuwa inasisitiza “kwamba wapiganaji shujaa wa Burkina Faso daima wamepiga vita kwa ufasaha na dhamira yao ya msingi ni kuwalinda watu, kutetea haki za binadamu, na kulinda watu waliodhulumiwa,” msemaji wa serikali alisisitiza.
Ouédraogo alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya ugaidi ni kipaumbele cha taifa kwa kiwango cha juu na yanafanywa kwa kuzingatia kikamilifu sheria za kitaifa pamoja na ahadi za kimataifa za Burkina Faso kuhusu haki za binadamu.