Rais wa Marekani Donald Trump amesema atafikia maamuzi ya kumaliza mashambulizi dhidi ya Iran, baada ya kukubaliana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Wiki iliyopita, Ikulu ya Marekani ilisema kuwa, huenda vita hivyo vikadumu kwa kati ya wiki nne hadi sita, huku Trump akisita kuweka wazi kikomo cha mashambulizi ya Marekani-Israel, dhidi ya Iran.
Mashambulizi hayo, ambayo yalianza Februari 28, yameua zaidi ya watu 1,200, akiwemo aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei.
"Nafikiri hili ni suala la makubaliano ya watu wawili. Nitafanya maamuzi katika muda muafaka," alisema Trump baada ya kuulizwa nafasi ya Netanyahu katika kumaliza mzozo dhidi ya Iran.
Hata hivyo, Trump hakuwa tayari kutoa maoni yake kuhusu uwezekano wa Israel kuendeleza mashambulizi dhidi ya Iran, iwapo Marekani itaamua kuacha.
"Sidhani kama ni muhimu sana kujibu hilo."
Mapema Jumapili, Baraza la Wataalamu la Iran, lilimchagua Mojtaba Khamenei kama Kiongozi Mkuu mpya, akichukua nafasi ya baba yake.














