Iran yatishia kuzuia usafiri wa meli katika Bahari ya Shamu ikiwa vikwazo vya Marekani vitaendelea
Marekani ilitangaza kuweka vikwazo katika njia ya bahari baada ya mazungumzo ya amani na Iran yaliyofanyika mwishoni mwa juma mjini Islamabad kutofaulu.
Jeshi la Iran lilionya kuwa litazuia meli zote za biashara kupitia Bahari ya Shamu, pamoja na maeneo ya Ghuba na Bahari ya Oman, ikiwa vikwazo vya majini vya Marekani vitaendelea.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano na kupitia televisheni ya taifa ya Iran, mkuu wa kamandi kuu la jeshi la Iran alisema kuwa kuendelea kwa zuio hilo, hasa ikiwa litahatarisha usalama wa meli za biashara na meli za mafuta za Iran, litachukuliwa kama hatua ya kwanza ya kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.
Alisisitiza kuwa vikosi vya kijeshi vya Iran havitaruhusu shughuli za uagizaji na usafirishaji bidhaa kuendelea katika maeneo ya Ghuba, Bahari ya Oman na Bahari ya Shamu iwapo hali hiyo itaendelea.
Taarifa hiyo imekuja siku moja baada ya Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) kutangaza kuwa imefanikiwa kusimamisha kabisa biashara ya baharini kwenda na kutoka Iran. Kwa mujibu wa CENTCOM, operesheni hiyo ilianza rasmi Jumatatu kwa kuzuia meli zote zinazoingia na kutoka katika bandari za Iran.
Kamandi hiyo ilieleza kuwa zuio hilo linatekelezwa bila upendeleo kwa meli za mataifa yote, zinazoelekea au kutoka katika bandari za Iran kupitia Ghuba na Bahari ya Oman.
Ripoti zinaonyesha kuwa vikosi vya majini vya Marekani vimeweka zuio kati ya Ghuba ya Gwadar na Ras al Hadd, eneo linaloshuhudia msongamano mkubwa wa meli tangu kuanza kwa operesheni hiyo.
Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza rasmi hatua hiyo Jumapili, akisema ni matokeo ya kushindikana kwa mazungumzo ya kidiplomasia na Iran.
Kwa mujibu wa CENTCOM, ndani ya saa 24 za kwanza tangu kuanza kwa operesheni hiyo, hakuna meli iliyofanikiwa kuvuka kizuizi hicho. Aidha, meli sita ziliripotiwa kufuata maelekezo ya vikosi vya Marekani na kurejea katika bandari za Iran.
Hata hivyo, taarifa za ufuatiliaji wa usafiri wa meli zinaonyesha kuwa harakati katika Mlango wa Hormuz bado zinaendelea, ingawa baadhi ya meli zilizokuwa zimeingia Ghuba ya Oman zililazimika kubadili mkondo na kurudi nyuma.
Takribani meli 15 zilipita katika mlango huo muhimu wa kimkakati ndani ya saa 24 zilizopita kufikia saa 0900 GMT, huku meli 10 kati ya hizo zikitoka nje ya mlango huo.
Miongoni mwa meli zilizoripotiwa kupita katika eneo hilo ni pamoja na meli za kubeba gesi na kemikali, meli za makontena za Iran, pamoja na meli za mafuta na mizigo kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu, China, Ugiriki, Brazil na India.
Taarifa za kampuni ya MarineTraffic pia zinaonyesha kuwa baadhi ya meli zilizowekewa vikwazo na Marekani zilifanikiwa kupita katika Mlango wa Hormuz, hali inayoashiria kuwa pamoja na zuio hilo, bado kuna harakati zinazoendelea katika njia hiyo muhimu ya kimataifa ya usafirishaji wa baharini.