Vita vya Israel- Marekani dhidi ya Iran vyatishia uhaba wa maji eneo la Ghuba

Mataifa mengi ya Ghuba huagiza kutoka nje kati ya asilimia 80 -90 ya chakula. Hii inawaweka katika utegemezi mkubwa wa njia muhimu ya usafiri wa meli za baharini na biashara ya kimataifa bila kukatishwa.

By
Israel na Marekani wameanzisha vita dhidi ya Iran / Picha : AP / AP

Huku vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran vikiendelea, habari za dunia zimekua zikiangazia zaidi masoko ya mafuta.

Lakini kuna janga jengine linalotishia eneo zima la Ghuba. Ukosefu wa maji safi na chakula.

Mnamo Machi 8 droni za Iran zinadaiwa kuharibu mitambo ya kuchuja chumvi nchini Bahrain ambayo husafisha maji ya bahari kuwa salama kwa kunywa.

Kwa Bahrain, miundombinu hiyo ni muhimu zaidi kwa sababu hutegemewa kwa utoaji wa takriban asilimia 90 – 95 ya maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu.

Na sio Bahrain peke yake, eneo lote hilo mitambo ya kusafisha maji ndio inayoshikilia uhai wake.

Katika nchi za UAE na Kuwait takriban asilimia 90 ya maji yote ya kunywa hutoka baharini.
Nchini Oman, kiasi hicho kinafikia asilimia 86. Saudi Arabia ni asilimia 70.

Historia imeonyesha namna mfumo huu unavyoweka kuwa hatarini. Wakati wa vita vya Ghuba vya 1990- 1991, mashambulizi dhidi ya mitambo ya kusafisha maji ya bahari nchini Kuwait, yalisababisha uhaba mkubwa wa maji ya kunywa.

Shambulio hili la Bahrain linafuatia mashambulio ya Marekani yaliyoharibu mtambo wa Iran wa kusafisha maji, na kukata usambazaji wa maji kwa vijiji kadhaa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameonya kuwa Marekani imeonesha mfano mbaya kwa kulenga miundombinu inayotumika kwa ajili ya huduma za wananchi.

Lakini maji ni sehemu moja tu hatari ya Ghuba, upatikanaji chakula pia upo hatarini.

Mataifa mengi ya Ghuba huagiza kutoka nje kati ya asilimia 80 -90 ya chakula. Hii inawaweka katika utegemezi mkubwa wa njia muhimu ya usafiri wa meli za baharini na biashara ya kimataifa bila kukatishwa.

Sasa kwa kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz, mojawapo ya njia muhimu zaidi za kupitisa mizigo imekatishwa.

Wachambuzi wa safari za meli wanakadiria kuwa zaidi ya meli 170 zilizosheheni takriban makontena 450 000 zimekwama katika eneo la Ghuba. Makampuni makubwa ya meli yamesitisha shughuli au kutangaza nyongeza ya gharama ya dharura.

Usitishaji wa safari za ndege pia umevuruga usafirishaji mizigo kupitia anga ikiwemo usafirishaji wa vyakula vinavyoharibika haraka kama nyama na bidhaa za maziwa ambazo kawaida husafirishwa kila siku.

Gharama za juu za usafirishaji na ucheleweshaji tayari zimesababisha kupanda kwa bei ya bidhaa hizi.

Serikali za Ghuba nazo zinajaribu kuwahakikisha wananchi wake usalama wa chakula.

Maafisa wa UAE, Qatar na Bahrain wanasema wana hifadhi ya kutosha ya kumudu miezi kadhaa ijayo.

Kuwait imepiga marufuku usafirishaji nje wa chakula ili kulinda hifadhi zake.

Lakini wachambuzi wanaonya kuwa iwapo mzozo utaendelea kwa muda mrefu, basi mataifa ya Ghuba yanaweza kuingia katika hatari nyengine itokanayo na uhaba wa chakula na maji safi.