Misri yaomboleza vifo vya watu 18 kufuatia ajali ya barabarani

Ajali za barabarani huua maelfu ya watu kila mwaka nchini Misri.

By
Ajali za barabarani zimekuwa hali ya kawaida nchini Misri kutokana na idadi kubwa ya ajali hizo. / / Reuters

Mamlaka za nchini Misri zimesema kuwa lori na gari dogo la mizigo ziligongana kwenye barabara kuu nchini humo mchana wa Alhamisi, na kusababisha vifo vya watu 18 pamoja huku wengine watatu wakheruhiwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Kazi, ajali hiyo ilitokea katika barabara ya 30 June Axis, kusini mwa mkoa wa Port Said. Watu wote waliopoteza maisha walikuwa wavuvi waliokuwa ndani ya moja ya magari hayo. Hata hivyo, bado haijafahamika wazi jinsi magari hayo yalivyogongana.

Waziri Mkuu Mustafa Madbouly alitoa salamu za rambirambi kwa familia za marehemu na kuagiza kutolewa kwa fedha za msaada kwa waathirika.

Gari hilo dogo lilikuwa likiwapeleka wavuvi hao kazini katika mabwawa ya kufugia samaki yaliyoko Port Said, mkoa wa pwani kaskazini-mashariki mwa Misri unaojulikana kwa shughuli kubwa za uvuvi. Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 6:30 mchana.

Eneo la ajali

Inaaminika kuwa waathirika wengi walikuwa wakazi wa mji na wilaya ya Matareya katika mkoa wa Dakahlia, kwa mujibu wa maafisa.

Picha zilizochapishwa kwenye ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Facebook wa Gavana wa Dakahlia zilionyesha athari za ajali hiyo, ambapo gari dogo lilikuwa limebanwa kati ya malori mawili makubwa ya mizigo.

Wakati huo huo, Gavana wa Port Said alitembelea eneo la ajali na kuwajulia hali majeruhi waliolazwa hospitalini ili kuhakikisha kuwa usafiri wa barabarani unarejea kwa hali ya kawaida na manusura wanapatiwa matibabu stahiki, kulingana na taarifa iliyotolewa na ofisi yake kupitia Facebook.

Ajali mbaya za barabarani huendelea kugharimu maisha ya maelfu ya watu kila mwaka nchini Misri. Mwendo kasi, hali mbaya ya barabara na udhaifu katika utekelezaji wa sheria za usalama barabarani ni miongoni mwa sababu kuu za ajali nyingi.