Uturuki yaendeleza misaada kwa Gaza licha ya vizuizi vya Israel: Erdogan
Licha ya vizuizi mbalimbali vinavyowekwa na Israel katika juhudi za misaada ya kibinadamu, tunatumia rasilimali zote tulizonazo kufikisha msaada Gaza,” amesema Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan.
Rais Erdogan amesema kwamba Uturuki inaendelea kusafirisha misaada ya kibinadamu kwenda Gaza licha ya “vikwazo mbalimbali vinavyosababishwa na Israel,” na akaonya kuwa usalama wa eneo hilo uko hatarini ikiwa ukaliaji wa Palestina unaendelea.
Akizungumza baada ya kikao cha Baraza la Mawaziri jijini Ankara siku ya Jumatatu, Erdogan alisisitiza kuwa hakuna nchi yoyote katika eneo hilo itakayokuwa salama ilhali damu ya Wapalestina itaendelea kumwagika na kupoteza ardhi yao.
Meli ya Wema 18 ya Hilali Nyekundu ya Uturuki, iliyobeba takriban tani 800 za misaada ikijumuisha blanketi za majira ya baridi, vyakula muhimu, na mahitaji mengine muhimu, iliwasili katika bandari ya al-Arish nchini Misri siku ya Ijumaa kuelekea Gaza.
Shirika hilo pia linaendelea kutoa vyakula kwa watu 35,000 kila siku ndani ya Gaza, na kusaidia hospitali na shughuli za afya zinazoendeshwa na Hilali Nyekundu ya Palestina.
Ingawa kumekuwepo na makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na Israel tangu Oktoba 10, Israel inaendelea kuyakiuka kila siku, na kusababisha vifo vya mamia ya Wapalestina.
Tangu Oktoba 2023, mashambulizi ya Israel yamewaua zaidi ya watu 69,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, kuwajeruhi zaidi ya 170,000, na kuifanya Gaza iwe sehemu ya kutowezekani kuishi.
Erdogan pia alisisitiza kwamba Uturuki inaendelea kuhimiza amani, haki, utulivu na ustawi wa pamoja katika mipaka yake ya kusini, kuanzia Iraq hadi Syria.