Serikali ya Sudan imeshtumu mashambulizi ya ndege isiyokuwa na rubani yaliyowaua raia wasiopungua 17 katika kijiji cha Shukeiri Jimbo la White Nile State, ikiilaumu wapiganaji wa RSF kwa shambulio hilo.
Katika taarifa, Waziri Mkuu Kamil Idris na maafisa wa serikali wamelitaja shambulio hilo kuwa la kikatili.
“Waziri Mkuu, Profesa Kamil Idris, na maafisa wa Serikali wanaeleza kusikitishwa kwao na kutuma salamu za rambirambi kwa mauaji ya mashahidi katika kijjiji cha Shukeiri Jimbo la White Nile, ambao roho zao zilichukuliwa kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan kutokana na mashambulizi yaliyofanywa na waasi na magaidi wa RSF,” kulingana na taarifa iliyotolewa na Shirika la Habari la Sudan.
Serikali inasema mashambulizi hayo yalilenga raia katika kijiji hicho na kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kuwawajibisha RSF.
‘Wanashambulia raia kwa makusudi’
Shambulio hilo lililenga shule ya sekondari na kituo cha afya huko Shukeiri siku ya Jumatano,na kuwaua watu wasiopungua 17, wengi wakiwa wanafunzi wa kike, na kuwajeruhi karibu watu 10, kulingana na maafisa wa afya.
Mtandao wa Madaktari wa Sudan unasema miongoni mwa walioathirika ni wanafunzi wa kike, walimu na wahudumu wa afya. Kundi hilo limeshtumu RSF kwa kushambulia kwa makusudi maeneo ya raia.
















