Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Felix Tshisekedi anasema kwa makundi yoyote yenye silaha, kama waasi wa M23, kushiriki katika majadiliano ya kitaifa haiwezekani kama kundi hilo litaendelea kupigana na serikali.
Katika hotuba kupitia televisheni ya taifa siku ya Alhamisi, kiongozi huyo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo anasema kuwa mazungumzo ya kitaifa yatakuwa “mchakato huru, ulioanzishwa na Wacongomani kwa ajili ya Wacongomani, kufanyika ndani ya nchi, na mahsusi kwa ajili ya maslahi ya Taifa.”
Tshisekedi ameongeza kuwa mazungumzo hayo “yatawaleta pamoja watu wa nchi yetu kwa lengo ambalo haliangazii mtu, chama, na maslahi binafsi: kulinda Jamhuri, kuhakikisha amani, umoja wa kitaifa, na kulinda maslahi yetu ya kimkakati”
DRC, ambayo iko Afrika ya Kati, imekabiliwa na mapigano hasa katika eneo la mashariki lenye utajiri wa madini.
Masharti ya kushiriki
Rais Tshisekedi aliwahakikishia kuwa, "Hakuna atakayetengwa kutokana na maoni yake, ukosoaji, au mtazamo wake wa kisiasa," lakini pia akaonya kuwa, "Hakuna mtu anaweza kupata nafasi kwenye mazungumzo wakati bado anapigana na serikali.’’
Majadiliano yatachukua hadi miezi mitatu, rais alisema, akiongeza kuwa matokeo yake yatatumika kama msingi wa "mazungumzo ya kitaifa" na "makubaliano ya kitaifa" kwa misingi ya "amani, umoja wa kitaifa na maslahi muhimu ya jamhuri".























