Rangi za vyama vya siasa zinavyohamasisha wapiga kura Uganda

Kila chama kilichosajiliwa kina utambulisho wake unaotumika kuhamashisha wapiga kura.

By
Uganda party colours / Others

Katika mfumo wa uchaguzi nchini Uganda, kama ilivyo katika nchi nyingine yoyote ya kidemokrasia, rangi na alama za vyama ni msingi wa utambulisho wa kisiasa na upigaji kura, haswa katika nchi ambayo uelewa wa sheria za kupiga kura unaweza kutofautiana kati ya watu wa tabaka moja hadi jengine.

Kila chama kilichosajiliwa kina utambulisho wake wa kipekee unaotumika kwenye kampeni kwanza kuvutia wafuasi, lakini pili, kuwasaidia wapiga kura kutambua alama za vyama siku ya upigaji kura.

Kwa sababu kampeni za kutafuta kura zinalenga watu kutoka kila pembe ya nchi, mara nyingi sio wapiga kura wote wanaojua kusoma na kuandika au kusoma vizuri majina ya vyama kwenye kura, alama na rangi huwasaidia watu kutambua chama wanachokipenda njia rahisi.

Vidokezo hivi huonekana kwenye karatasi za kupigia kura, mabango ya kampeni, mavazi na bendera - na mara nyingi huwa na maana zaidi zinazohusiana na historia, dhamira au maadili ya chama.

Utambulisho wa vyama kwa rangi zao

1. National Resistance Movement (NRM) - Rangi ya njano katika mapambo na bidhaa za kampeni zikiwemo fulana, leso au khanga, suti, kofia, bendera za vyama na magari.

NRM ni chama tawala cha muda mrefu cha Uganda, kinachoongozwa na Rais Yoweri Museveni, madarakani tangu 1986. Alama ya basi inaonyesha maendeleo, uwezo wa kwenda mbele na ufanisi, ikionyesha msisitizo wa chama juu ya utulivu na uongozi wa muda mrefu.

2. National Unity Platform (NUP) - Rangi: Nyekundu, mara nyingi huunganishwa na nyeupe na bluu katika chapa rasmi.

NUP ni moja wapo ya vyama vikuu vya upinzani kinachoongozwa na Robert Kyagulanyi Ssentamu (pia anajulikana kama Bobi Wine) imehusishwa sana na msingi wa nguvu na vijana wa NUP. Kinaonekana kuwakilisha kujitolea kwa vijana katika mapambano na msukumo wa kuleta mabadiliko.


3. Forum for Democratic Change (FDC) - Maarufu kwa rangi ya bluu.

Pamoja na alama yake maarufu ya Ufunguo, inakusudiwa kuwakilisha fursa na uwezo wa kufungua, sambamba na ujumbe wa chama kuhusu kufungua nafasi ya kisiasa na kiuchumi kwa wananchi.

4. Democratic Party (DP) - Maarufu kwa rangi ya Kijani, pia wakati mwingine hujumuisha rangi nyengine kwenye nyenzo za kampeni.

Kijani pamoja na nembo yake ya jembe zinasisitiza mizizi ya kilimo na uhusiano na jamii za vijijini, ambazo kihistoria zimekuwa na wafuasi wa DP.

  1. Uganda People’s Congress (UPC) Kijadi rangi zake ni nyeusi, nyekundu, na buluu katika historia ya chama. Kwa mujibu wa utambulisho wa chama, rangi zao zinaonesha ushirikishwaji na juhudi za pamoja.
  2. Uganda Federal Alliance (UFA) - Inajitambulisha kwa rangi ya buluu na njano. Ni miongoni mwa vyama vidogo nchini Uganda, kilichoanzishwa mwaka 2010 na kinatumia zaidi nembo ya twiga kwenye bendera yake.
  3. People's Progressive Party (PPP) - Rangi zake ni mchanganyiko wa nyekundu, chungwa, buluu na nyeupe. Kwanza kilikuwa na jina la National Progressive Movement (NPM) kabla ya kuwa PPP kuanzia Disemba 2005.