Maafisa wa Pwani wa Mauritania wanasema wamewaokoa wahamiaji 260 katika maboti mawili, ikiwemo watoto 17, kutoka pwani ya bahari ya Atlantiki siku ya Jumapili.
Wahamiaji walikuwa ndani ya maboti mawili ambayo yalianza safari yake mjini Banjul, Gambia na walikuwa katika hali mbaya baada ya kuishiwa na chakula na mafuta na matatizo ya kutafuta njia, maafisa hao walisema.
Walionekana kutoka mji mkuu wa Nouakchott, baada ya kuwepo baharini kwa karibu siku saba, waliongeza.
Miongoni mwa wale waliookolewa ni raia 132 wa Senegal, 120 wa Gambia, wanne kutoka Guinea na wengine kadhaa kutoka Afrika magharibi, taarifa kutoka kwa maafisa hao ilisema.
Pamoja na watoto hao 17, kulikua na wanawake 61 ndani ya maboti hayo, taarifa iliongeza.
Maelfu ya vijana mara nyingi wamekuwa wakitumia njia hiyo hatari ya Atlantiki kwa maboti yaliyojaa na makuukuu kwa lengo la kufika Ulaya kupitia visiwa vya Canary vya Hispania.
Wengi wanakimbia umaskini na hutumia njia hizo kutokana na mataifa ya Ulaya kuweka masharti magumu ya kupata viza na kuimarisha ulinzi kwenye mipaka yao.





















