Baraza la Maaskofu Tanzania lataka uwajibikaji kwa waliohusika na mauaji ya waandamanaji

Maaskofu wa Tanzania wamelaani mauaji hayo na kuitisha uchunguzi unaoshirikisha wadau wa ndani na wa nje huku wakiiomba serikali iwe tayari kutekeleza ripoti itakayotolewa

By
Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na wote waliohusika na mauaji WAWAJIBIKE au KUWAJIBISHWA na mamlaka zao za uteuzi. / Ukurasa wa X

Baraza la Maaskofu Tanzania limelaani vikali mauaji ya waandamanaji wakati na baada ya uchaguzi mkuu kama uovu mkubwa na chukizo kwa Mungu.

Kupitia kwa Rais wa Baraza hilo na Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, Mhashamu Wolfgang Pisa baraza hilo limesisitiza kuwa maandamano ni haki na sio kila mandamano ni uhalifu.

‘‘Kuandamana ni haki ya raia kama njia ya kufikisha ujumbe au malalamiko ikiwa njia ya mazungumzo imeshindikana chamsingi yawe maandamano ya amani,’’ ilisem ataarifa hiyo. ‘‘Inasikitisha kuona kuwa Waandamanaji waliojitokeza siku ya uchaguzi wote waliwekwa katika mwavuli wa uhalifu. Adhabu ya mwandamanajii siyo kuuawa.’’ iliendelea kusema taarifa.

Baraza hilo limekariri baadhi ya malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa baadhi ya raia kuhusu matukio ya waziwazi ya mauaji, utekaji, kupigwa na kuumizwa kwa raia.

Sababu zilizochangia maandamano

Serikali imekuwa ikikanusha madai haya japo vyombo vya usalama vimetoa taarifa ya kufanyia uchunguzi visa maalum vilivyotajwa vya utekaji.

Maaskofu hao wameelezea sababu kadhaa wanazoamini zilichangia kuzuka maandamano na rabsha ikiwemo kudorora usalama, kukiukwa taratibu za demokrasia juu ya kuwachagua viongozi na ukosefu wa usikizi kwa malalamiko ya wananchi.

Baraza hilo la Maaskofu limeorodhesha matakwa yao katika taarifa hiyo ikiwemo kuwataka wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na wote waliohusika na mauaji wawajibike au kuwajibishwa na mamlaka zao za uteuzi.

Katika orodha ya vitu vinane walivyotaka vifanyike, pia wameitisha wale wote waliokamatwa kwa hila kabla na baada ya uchaguzi na kuwekwa mahabusu au mahali pasipojulikana waachiwe huru na bila ya masharti yoyote.

Tume ya kuchunguza mauaji

‘‘Katiba mpya na utawala wa sheria vimekuwa kilio cha muda mrefu hapa nchini. Mchakato wa Katiba mpya yenye kujali utu, usawa, haki, ukweli kwa wote uanze kwa kukushirikisha wadau wote. Ili tusirudi tena katika machafuko na nchi iongozwe katika utawala wa sheria.’’ wameongeza.

Tanzania imetumbukia katika lawama na shutuma za kimataifa tangu Oktoba 29, ambapo maandamano ya kupinga uchaguzi mkuu yalikabiliwa kwa nguvu kupita kiasi, huku vijana wengi wakidaiwa kuuawa kw akupigwa risasi na vyombo vya uslama.

Awali uongozi wa serikali ulikanusha madai kuwa Watanzania waliuawa, lakini baadaye, katika hotuba ya kwanz aya kulifungua bunge Rais Samia Suluhu Hassan, alitangaza kuteua tume itakayofanya uchunguzi huku akitoa pole kwa waliofiwa na waliojeruhiwa katika maandamano.