| Swahili
ULIMWENGU
2 dk kusoma
Ufaransa yaishutumu Iran kwa kushambulia mifumo ya majokofu katika maduka
Ufaransa imeishutumu Walinzi wa Mapinduzi wa Iran kwa kufanya mashambulizi ya kimtandao na kutishia kuweka vikwazo zaidi kutoka Umoja wa Ulaya, huku ikimwita balozi wa Iran kwa mashauriano kufuatia mashambulizi hayo.
Ufaransa yaishutumu Iran kwa kushambulia mifumo ya majokofu katika maduka
Wateja wanaingia katika duka kubwa la Intermarché karibu na Paris, baada ya shambulio la kimtandao dhidi ya majokofu nchini Ufaransa. /

Maafisa wa Ufaransa siku ya Jumatatu waliwashutumu Walinzi wa Mapinduzi wa Iran (IRGC) kwa kuhusika na mashambulizi ya mtandaoni yaliyosababisha hitilafu katika mifumo ya majokofu katika maduka makubwa nchini Ufaransa mwezi uliopita. Maafisa hao walisema Iran itawajibishwa kutokana na tukio hilo.

Mashambulizi hayo ya kimtandao, yaliyolenga mamia ya maduka makubwa nchini Ufaransa mwanzoni mwa mwezi Oktoba, yalikuwa miongoni mwa mashambulizi yaliyosababisha athari kubwa zaidi katika vita vya Iran vilivyoanza mwezi Februari. Vita hivyo vimekuwa vikihusishwa na matukio mbalimbali ya hapa na pale ya madai ya hujuma na uvurugaji wa mifumo ya kidijitali.

Matukio mengine yaliyoripotiwa ni pamoja na mashambulizi ya kimtandao dhidi ya mfumo wa usafiri wa Los Angeles, Marekani mwezi Machi, vituo vya kusafisha maji nchini Marekani mwezi Julai, pamoja na meli zilizokuwa zikielekea Marekani mwezi Agosti.

Ujumbe wa Iran katika Umoja wa Mataifa haukutoa ufafanuzi kuhusu tuhuma hizo. Iran imekuwa ikikanusha mara kwa mara kuhusika na operesheni za kimtandao.

Tangazo la Ufaransa lilitolewa dakika chache tu baada ya shirika la habari la Reuters kufichua kuwa wachunguzi wakiituhumu Iran kuhusika na mashambulizi hayo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, alisema kuwa balozi wa Iran nchini Ufaransa ameitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa kwa mazungumzo kuhusu suala hilo.

Aidha, Barrot alitishia kuwa Umoja wa Ulaya unaweza kuiwekea Iran vikwazo zaidi.

CHANZO:Reuters