Zaidi ya watu 500,000 waandamana kuiunga mkono Palestina mjini Istanbul katika siku ya Mwaka Mpya

Yakiongozwa na viongozi wa kidini na kiraia, mkutano wenye kauli mbiu ya “Hatuwezi Kukaa Kimya” uliwakutanisha washiriki kutoka zaidi ya mashirika 400 ya kijamii.

By
Walioshiriki maandamano hayo walipeperusha mabango yaliyoandikwa "Haki kwa Palestina" na kulaani vitendo vya Israel. / / AA

Takribani watu 520,000 walikusanyika mapema Alhamisi, Siku ya Mwaka Mpya, katika Daraja la Galata mjini Istanbul kwa maandamano makubwa ya kuunga mkono Palestina, yaliyoandaliwa chini ya mwavuli wa Humanity Alliance na National Will Platform.

Maandamano hayo, yaliyofanyika kwa kushiriki kwa zaidi ya mashirika 400 ya kiraia na kuongozwa na Wakfu wa Vijana wa Uturuki (TUGVA), yalifanyika chini ya kaulimbiu: “Hatutaogopa, hatutakaa kimya, hatutasahau Palestina.”

Walioshiriki maandamano hayo walitoa wito wa kukomeshwa kwa mauaji ya halaiki huko Gaza.

Kabla ya tukio hilo, raia walikusanyika kabla ya swala ya alfajiri katika misikiti mikubwa kote Istanbul, ikiwemo Msikiti Mkuu wa Ayasofya, Sultanahmet, Fatih, Suleymaniye na Msikiti Mpya wa Eminonu. Wengi walibeba bendera za Uturuki na Palestina walipokusanyika katika viwanja vya misikiti kuonyesha mshikamano wao na Palestina.

Licha ya baridi kali, idadi ya waliojitokeza ilikuwa kubwa. Hatua kali za kiusalama zilichukuliwa, hasa katika Uwanja wa Sultanahmet, ambako washiriki pia walipewa vinywaji vya moto.

Baada ya swala ya asubuhi, waandamanaji walitembea kwa miguu kuelekea Daraja la Galata, wakiungana na mawaziri, maafisa wakuu wa serikali na watu waliomo katika itifaki rasmi ya taifa. Ratiba rasmi ilianza saa 8:30 asubuhi kwa saa za eneo (05:30 GMT).

Bango kubwa lenye picha ya “Hanzala,” mhusika maarufu aliyeundwa na marehemu mchora katuni wa Kipalestina Naji al-Ali na anayehusishwa kwa karibu na harakati za Palestina, lilining’inizwa kwenye jengo lililokuwa nyuma ya jukwaa kuu la waandishi wa habari.

Tukio hilo pia lilijumuisha maonyesho ya wasanii na wanamuziki mashuhuri kimataifa, akiwemo mwimbaji mwenye asili ya Lebanon na raia wa Uswidi Maher Zain, msanii wa Mturuki Esat Kabakli, na bendi ya Grup Yuruyus.

‘Tulianza mwaka mpya kwa kuiombea Palestina’

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa maandamano, Bilal Erdogan, mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Wakfu wa Ilim Yayma na mjumbe wa Baraza Kuu la Ushauri la TUGVA, alisema kuwa mwaka mpya umeanza kwa maombi kwa ajili ya Palestina na kwamba kukusanyika misikitini asubuhi ya kwanza ya mwaka kuna maana kubwa ya kiroho.

Erdogan alisema ni muhimu kutambua nguvu ya kimaadili na kiroho ya kukutana misikitini alfajiri na kutoa maombi ya pamoja kwa mwaka mpya, akiongeza kuwa taifa linaamini sana katika umoja huo.

“Kwa upande mmoja, tunawaombea waliodhulumiwa huko Palestina. Kwa upande mwingine, bila shaka, tunawakumbuka mashahidi wetu. Wakati huo huo, tunaomba kwa pamoja kwamba mwaka 2026 ulete kheri kwa taifa letu zima na kwa Wapalestina waliodhulumiwa,” alisema.

“Ningependa kuwashukuru kwa dhati wote walioshiriki, wote waliokunja mikono yao katika maombi, na wote waliounga mkono maombi haya,” aliongeza Erdogan.

Akirejelea ongezeko la idadi ya washiriki katika tukio la kila mwaka, Erdogan alisema idadi ya wanaoshiriki inaongezeka kila mwaka, jambo linaloonyesha nguvu ya maadili ya pamoja katika jamii.

“Kila mwaka, ukilinganisha na uliotangulia, tunahisi kuwa asubuhi hii inaashiria ushiriki mpana zaidi na kwamba, kama taifa, tunatambua jinsi msingi wetu wa pamoja ulivyo imara. Hili linatufurahisha sana,” alisema.

Akieleza matumaini kwa mwaka ujao, Erdogan aliongeza: “Mwenyezi Mungu atujaalie, na awezeshe taifa hili kuona msimamo huu kama chanzo cha fahari mwaka huu, awape uhuru ndugu zetu na dada zetu wa Kipalestina, na atujalie uhuru wa Quds (Jerusalem).”

Mwenyekiti wa TUGVA atoa hotuba kali

Akizungumza katika maandamano hayo, Mwenyekiti wa TUGVA, Ibrahim Besinci, alisema ukubwa wa umati uliokusanyika unaakisi msimamo wa pamoja wa kimaadili dhidi ya vurugu zinazoendelea Palestina.

“Leo, kuna mamia ya maelfu hapa. Kuna taifa lenye heshima limesimama imara dhidi ya mauaji haya ya halaiki,” alisema Besinci.

Akilihutubia umati katika Daraja la Galata, alisema: “Leo, kuna mamia ya maelfu hapa. Kuna taifa lenye heshima limesimama imara dhidi ya mauaji haya ya halaiki. Kuna maombi ya waliodhulumiwa na urithi wa mashahidi wetu.”

Akiitaja Daraja la Galata kama “jukwaa la dhamiri,” Besinci alisema limegeuka kuwa jukwaa la kimaadili kwa watu kutoka miji, lugha na matabaka mbalimbali ya maisha.

“Kutoka katika jukwaa hili tukufu, nawapa salamu zangu za dhati watu wasio na hatia na walio jasiri wa Palestina, wana wa heshima wa Gaza, mioyo imara ya Ukingo wa Magharibi, na wamiliki halisi wa Jerusalem ya Mashariki,” alisema.

Besinci pia aliwakumbuka maafisa watatu wa polisi — Ilker Pehlivan, Turgut Kulunk na Yasin Kocyigit — waliouawa siku tatu zilizopita wakati wa operesheni dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh katika jimbo la Yalova, kaskazini-magharibi mwa nchi.

Akitaja takwimu za uharibifu huko Gaza, Besinci alisema kuwa katika kipindi cha miezi 27 iliyopita, tani 210,000 za mabomu zimetumiwa dhid ya Gaza, raia 70,000 wameuawa, familia 2,600 zimefutwa kabisa kwenye sajili ya idadi ya watu, na familia 5,000 zimebakiwa na mwanafamili mmoja tu aliyehai.

Aliongeza kuwa Wapalestina 45,000 wamekatwa viungo na huku wengine 12,000 wamefungwa.

“Kwa kuweka wazi zaidi, mbele ya macho ya dunia nzima, watu wamefutwa si tu kutoka kwenye ramani, bali kutoka kwenye maisha,” alisema Besinci.

Wadau wa michezo watoa uungaji mkono

Jumatano, jukwaa la pamoja la mashirika ya kiraia lilifanya mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya Wakfu wa Vijana wa Uturuki. Wakati wa mkutano huo, wenyeviti wa vilabu za Besiktas, Galatasaray na Trabzonspor, pamoja na mjumbe wa bodi ya Fenerbahce Ertan Torunogulları, walitangaza hadharani uungaji mkono wao kwa maandamano hayo. Klabu nyingine kadhaa za michezo pia zilitoa wito kwa umma kushiriki.

Katika mkutano huo huo, Bilal Erdogan alisema kuwa “zaidi ya watu 70,000 na angalau watoto 20,000 wameuawa katika mauaji ya halaiki ya Gaza tangu Oktoba 2023.”

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, angalau watu 414 wameuawa na zaidi ya 1,100 wamejeruhiwa tangu makubaliano ya kusitisha mapigano ya Oktoba 10 yaliyosimamisha vita vya Israel vilivyoendelea kwa miaka miwili.

Maonesho ya ukuzaji wa sanaa na utamaduni uliangaziwa

Kama sehemu ya ratiba, maombi kwa ajili ya Wapalestina yaliendelea katika jukwaa lililowekwa kwenye Daraja la Galata.

Aidha, kazi ya sanaa iliyopewa jina “Roots” ilizinduliwa kwenye daraja hilo ili kuangazia kile waandaaji walichokitaja kuwa ni kulengwa kwa utamaduni na sanaa huko Gaza.

Kwa mujibu wa taarifa ya TUGVA, kazi hiyo ya sanaa ilibuniwa kuashiria kumbukumbu na upinzani mbele ya uharibifu wa kitamaduni. Mti wa mzeituni unaochipuka kutoka kwenye kifusi uliwakilisha mizizi ya ukaidi na jaribio la kufuta kumbukumbu ya pamoja, huku viti vilivyopinduliwa, ala za muziki zilizotawanyika, vitabu na kamera vikionyesha juhudi za kunyamazisha uendelezaji wa kitamaduni.

Kauli “Tutabaki Hapa,” iliyoandikwa kwa lugha tatu, ilisisitiza dhamira ya upinzani wa kitamaduni na kibinadamu.