Bei ya mafuta ya petroli imepanda kwa kiwango kikubwa nchini Tanzania, huku nishati hiyo muhimu ikiuzwa kwa Dola 1.47 (Shilingi za Kitanzania 3,820) kwa lita katika Jiji la Dar es Salaam toka kiasi cha Dola 1.10 (Shilingi za Kitanzania 2,864) kwa mwezi Machi.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji nchini Tanzania (EWURA), Aprili 1, 2026, gharama hizo zimeongezeka kutokana na mabadiliko ya soko la kimataifa, likiwemo ongezeko la bei ya mafuta ghafi na changamoto za usafirishaji.
Aidha, hali ya kisiasa na kiusalama duniani, hususan mvutano unaoendelea kati ya mataifa mbalimbali, imechangia kuvuruga upatikanaji na usambazaji wa mafuta katika masoko ya kimataifa, kulingana na EWURA.
Bei hizo mpya zitaanza kutumika kuanzia Aprili Mosi katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara.
Hata hivyo, EWURA imewataka wanachi kutumia nishati kwa uangalifu na kuzingatia njia mbadala za kupunguza matumizi, huku EWURA ikisisitiza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa soko la dunia ili kulinda maslahi ya watumiaji wa ndani.















