Rais Samia aitaka Tanzania kuongeza akiba ya mafuta huku mgogoro wa Mashariki ya Kati ukiendelea

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati umeanza kuathiri uchumi wa nchi, huku bei ya mafuta ikipanda kwa asilimia 13.

By
Rais Samia amesema mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati umeanza kuathiri uchumi wa nchi, huku bei ya mafuta ikipanda kwa asilimia 13. / TRT Afrika Swahili

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema mgogoro unaoendelea Mashariki ya Kati umeanza kuathiri uchumi wa nchi, huku bei ya mafuta ikipanda kwa asilimia 13. Ameeleza wasiwasi wake juu ya mustakabali wa uchumi iwapo hali hiyo itaendelea.

Rais ametoa kauli hiyo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa matanki ya kupokea na kuhifadhi mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, akisema mradi huo utaongeza uwezo wa uhifadhi na kuifanya Dar es Salaam kuwa kitovu cha biashara ya nishati Afrika Mashariki.

Hatua hiyo imekuja muda mfupi baada ya Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje kutangaza kuwa inafuatilia kwa karibu hali ya usalama katika eneo la Mashariki ya Kati, na kuwashauri raia wa Tanzania wanaoishi au wanaopanga kusafiri katika nchi za Bahrain, Israel, Kuwait, Qatar na Falme za Kiarabu (UAE) kuchukua tahadhari.

Serikali imewataka kuepuka safari zisizo za lazima, kubaki majumbani inapowezekana, kufuata maelekezo ya mamlaka za maeneo husika, kuepuka maeneo ya kijeshi, kutumia njia rasmi za mawasiliano, na kuhifadhi nyaraka muhimu kwa usalama.

Wizara hiyo imeeleza kuwa pamoja na Misheni za Kidiplomasia itaendelea kutoa taarifa na usaidizi wa kibalozi kadri hali itakavyoruhusu.