Raia wa Kenya anayetuhumiwa kuwasajili watu kushiriki katika vita vya Urusi nchini Ukraine akamatwa

Polisi walisema kuwa Festus Omwamba alikamatwa karibu na mpaka wa Ethiopia akijaribu kutoroka baada ya kurudi kutoka Urusi.

By
Festus Omwamba alikamatwa kwa tuhuma za kuwasafrisha watu kinyume na sheria. / Wengine / Others

Polisi nchini Kenya wamemkamata mwanamume anayetuhumiwa kuhusika katika mpango unaodaiwa kuwalaghai Wakenya kwa ahadi za kazi nchini Urusi, na baadaye kuwapeleka kupigana upande wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Festus Omwamba alikamatwa kwa tuhuma za kusafirisha watu kinyume na sheria katika mji wa Moyale, kaskazini mwa Kenya karibu na mpaka wa Ethiopia, na kusafirihwa jijini Nairobi.

Msemaji wa polisi Michael Muchiri alisema Omwamba alikuwa mafichoni baada ya kurejea kutoka Urusi.

Omwamba, ambaye alitambuliwa na waajiriwa watatu wa Kenya waliozungumza na Shirika la Habari la Associated Press, alitoweka baada ya familia kuanza kuandamana kupinga kutoweka na kuawa kwa ndugu zao katika vita vya Ukraine.

Zaidi ya watu elfu moja walisajiliwa

Serikali ya Kenya wiki iliyopita ilisema zaidi ya Wakenya 1,000 waliandikishwa kupigana upande wa Urusi nchini Ukraine na kwamba angalau Wakenya bado walikuwa vitani, 39 walikuwa wamelazwa hospitalini, 28 hawajulikani walipo, na wengine walikuwa wamerudi nyumbani. Huku mtu mmoja alithibitishwa kufariki dunia.

Ripoti ya kijasusi iliyowasilishwa katika Bunge la Kenya na Kiongozi wa Wengi, Kimani Ichung’wah, ilisema maafisa wa serikali za Kenya na Urusi walishirikiana na mawakala wa ajira wasio waaminifu kuwasajili Wakenya kwenda kupigana.

Ubalozi wa Urusi jijini Nairobi ulikanusha madai hayo, ukisema katika taarifa siku ya Alhamisi kwamba haujawahi kutoa viza kwa mtu yeyote aliyekusudia kusafiri kwenda Urusi kupigana nchini Ukraine.

Uliongeza: “Serikali ya Urusi halizuii raia wa nchi za kigeni kujiunga kwa hiari katika jeshi lake.”

Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, tarehe 9 Februari alisema atasafiri kwenda Urusi kwa kile alichokiita “njia ya kidiplomasia ya kudhibiti taasisi zenye utata zinazolaghai watu katika mkasa huu.”

Hatua kubwa

Kukamatwa kwa Omwamba ni hatua kubwa katika jitihada za serikali kuzuia usajili wa Wakenya kwenda kupigana nchini Ukraine.

Mmoja wa waajiriwa aliyekimbia vitani kutafuta hifadhi katika Ubalozi wa Kenya nchini Urusi, na baadaye kusaidiwa kurejea nyumbani, John Kamau, aliliambia Shirika la Habari la AP kwamba alikutana na Omwamba katika nyumba moja jijini Nairobi ambako waajiriwa wengine waliokuwa wakisubiri kusafiri kwenda Urusi walihifadhiwa.

Mwajiriwa mwingine, aliyeomba kutotajwa jina, alisema Omwamba aliepuka kuwasiliana na waajiriwa kwa ujumbe mfupi wa maandishi na badala yake aliwapigia simu au kukutana nao ana kwa ana.

Mwajiriwa huyo alisema alijiandikisha baada ya kuambiwa atapata kazi ya ufundi bomba nchini Urusi, lakini alipowasili, pasipoti yake ilichukuliwa na alipelekwa katika kambi ya kijeshi kwa siku chache kabla ya kupelekwa vitani.

Waajiriwa wote walisema Omwamba alisimamia maombi yao ya viza za utalii na ununuzi wa tiketi, na wiki mbili baada ya mawasiliano ya kwanza, walipokea viza na kusafiri kwenda Urusi.