Ramadhan Uganda: Wito wa amani
Viongozi wa dini ya Kiislamu nchini Uganda wanawataka waumini kuutumia mwezi huu mtukufu wa Ramadhan kuungana na kusameheana hasa baada ya kipindi kigumu cha mvutano kilichosababishwa na Uchaguzi Mkuu wa urais wa tarehe 15 Januari 2026.
Ni siku yenye shughuli nyingi hapa kwenye Msikiti wa Swiddik, katika mji mkuu wa Uganda, Kampala.
Hajji Habib Mboya anaandaa chakula kwa ajili ya futari.
Anasema anawaza sana jinsi nchi inavyoweza kurudisha amani baada ya mvutano wa kisiasa uliosababishwa na Uchaguzi Mkuu.
“Tunawaomba Waislamu wote; hata wale ambao sio Waislamu, Wakristo, uchaguzi umeisha. Tunawaomba tuungane na kuliendeleza taifa letu,” Hajji Mboya anaiambia TRT Afrika, huku akiendelea na maandalizi yake ya chakula.
Kula pamoja imekuwa desturi katika msikiti huu, ukilenga hasa wale ambao hawana uwezo wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
“Tunafanya kazi pamoja na kuendeleza nchi. Tunawaomba Waislamu wote wa chama cha NRM na chama cha NUP kuungana pamoja,” anasema.
Wito wa Rais baada ya Uchaguzi Mkuu
Rais wa Uganda Yoweri Museveni katika hotuba yake kwa taifa hivi karibuni alitoa wito kwa wananchi 'kuacha ubaguzi na kutenda haki kwa wote, hata kwa walio katika vyama vya upinzani.'
Hii ni baada ya mvutano wa kisiasa kuendelea nchini baada ya Uchaguzi Mkuu wa 15 Januari 2026 ambapo alitangazwa kuwa mshindi.
Kiongozi wa chama cha upinzani cha NUP, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine ambaye alionekana kuwa mshindani wake wa karibu amejificha tangu wakati huo akidai kuwa maisha yake yapo hatarini.
Rais Museveni alisisitiza kwamba “raia wote lazima waungane kwa ajili ya maridhiano yenye kanuni na kuzungumza kuhusu makosa yaliyoonekana wakati wa uchaguzi na kuyatatua kwa mustakabali mwema.”
Na sasa waumini wengi wa Kiislamu mwaka huu wanasema Ramadhan imekuja kwa wakati muafaka, ili taifa liombee uponyaji.
"Usikate tamaa wakati ungali hai, Mwenyezi Mungu alitujaalia mwezi huu wa Ramadhan tutubu, tutende mema, uamke usiku uswali, umfikishie haja zako naye atakujibu maombi yako," Abdalla Katumba, mkazi wa Kampala anaiambia TRT Afrika huku akijitayarisha kuingia msikitini.
Ibada ambayo anahudhuria yeye inaongozwa na Imam Ismail Ssemakula.
Ujumbe wa imam leo ni umuhimu wa umoja.
"Umoja ndiyo njia pekee ya kusonga mbele badala ya utengano, tukiachana na hayo maendeleo yanakuwa madogo, kuna mambo mengi yanatutenganisha lakini tunaweza kupambana nayo na kuungana tena,” Imam Ismail Ssemakulawa wa Masjid Swiddik amesema.
Na wanapokusanyika baada ya ibada kama jumuiya kufuturu, Habib na waumini wengine hapa wanaamini kwamba hii ni hatua kubwa kuelekea kutafakari kwa pamoja na kufikia umoja ambao nchi inatafuta.