Mke wa Rais wa Uturuki Emine Erdogan amekutana na wenza wa viongozi wa NATO katika majadiliano yenye mada ya "Watoto, Teknolojia na Usalama: Kulinda Kizazi Kijacho" pembeni mwa kongamano la NATO jijini Ankara Julai 8.
Erdogan aliwasalimia wenza wa viongozi hao mmoja baada mwingine yeye mwenyewe walipowasili katika Kasri la Cankaya.
Brigitte Macron, Mke wa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, amesema kuwa Ufaransa inajaribu kupunguza muda wa watoto kutumia simu wakiwa shuleni.
Macron alisema, "Kwa mfano, unachokisoma kwenye simu hakina athari sawa na kile unachokisoma kwenye kitabu. Kwa nini tunaleta vikwazo hivi? Kwa sababu tumegundua vitu fulani. Kwa sababu siyo sawa na mfumo wa mafunzo. Hatutaki (watoto) waanze kutumia simu wakiwa na umri mdogo."
Macron alieleza kuwa watoto wanatizama video bandia "ambazo zinaweza kuwahadaa," akiongeza, "Tunahitaji kuangazia mustakabali wetu. Tatizo tunalikodolea macho. Tunaliona lilikuwa. Na tunahitaji kulishughulikia."
Akizungumzia kuhusu Akili Unde, Macron alisema kuwa wanafunzi wa Ufaransa wanakumbushwa kuwa waangalifu kuhusu kuchagua taaluma, akisema, "Tunawaambia wawe makini katika kuchagua tasnia. Mambo yanabadilika kwa haraka sana. Kuna hali ya wasiwasi. Hatuwezi kujua muelekeo ni upi kwa sasa."
Diana Nausediene, mke wa Rais wa Lithuania, alieleza kuwa kila mtu alikubali kuwa dunia ya sasa ya teknolojia lazima iwe salama kwa watoto, akiongeza kuwa watoto lazima walindwe kutokana na unyanyasaji wa mtandaoni, upotoshaji wa taarifa na kurubuniwa.
Nausediene alisisitiza kuwa watunga sera lazima waungane na wadau wengine, akisema, "Tunakabiliwa na changamoto kubwa, na tunahitaji juhudi za kimataifa."
Akieleza kuwa wanachama wa NATO wanatakiwa kushirikiana kulinda vizazi vya watoto dhidi ya kurubuniwa, Nausediene alisema kuwa watoto "ni kundi lililoko kwenye hatari zaidi ya kupewa taarifa za kupotosha."
Mke wa Rais wa Finland, Suzanne Innes-Stubb, alisema ulimwengu wa kidijitali una faida za msingi na watoto wanatumia mitandao ya kijamii kuwasiliana, kujumuika na watu, kujifunza, na kupata taarifa.
Innes-Stubb alieleza kuhusu hatari inayohusishwa na kueneza taarifa potofu, akieleza kuwa kwa watoto wengi, dunia ya kidijitali ni "sehemu ya maisha ya kila siku" na kuwa watoto wengi wanajiunga na mitandao ya kijamii kila dakika.













