Kinachofanya kupooza usingizini kuwa zaidi ya tatizo la kiafya

Kupooza usingizini huhusisha sayansi na imani za kiroho, na kuonyesha jinsi tamaduni zinavyoathiri namna watu wanavyoitikia hali inayochanganya kati ya uhalisia, ndoto, na udhaifu wa kibinadamu mbele ya hofu.

By Firmain Eric Mbadinga
Wataalamu wa afya ya akili wanakadiria kwamba angalau 30% ya idadi ya watu duniani wanpooza usingizibi./ Picha: Women's Health / Others

Mpendaga Karla, akiwa amelala kitandani, anajikuta amepooza bila uwezo wa kusogea au kuomba msaada, ingawa yuko macho.

Kitu fulani ndani yake kinachukua udhibiti katika hali inayohisiwa kama ndoto na uhalisia kwa wakati mmoja. Anapofanikiwa hatimaye kujinasua katika hali hiyo, Karla hujikuta amechoka, mwenye wasiwasi na aliyeudhika.

Mjasiriamali huyu wa miaka 40, mkazi wa mji mkuu wa Gabon, Libreville, anaelewa hali hili vyema sana.

“Kwetu sisi, hizi ni shambulio za kichawi, si kingine,” anasema Karla. “Hutokea mtu anapokushambulia katika ulimwengu wa kiroho. Siyo jambo la kubeza. Iliponitokea, sikuweza hata kusogea, ingawa nilikuwa na fahamu hata nikiwa usingizini. Ni kama jinamizi ambapo ninakimbizwa au kushambuliwa.”

Karla anaelezea kupooza usingizini, hali ambayo wataalamu wa afya ya akili wanakadiria huwapata angalau asilimia 30 ya watu duniani. Wengine asilimia 70 wamewahi kuiona kwenye filamu: wahusika wakinasa ndani ya ndoto za kutisha bila uwezo wa kujilinda au kuamka.

Tafsiri za kitamaduni

Barani Afrika, kama ilivyo sehemu nyingi duniani, watu wengi huitafsiri kupooza usingizini kama tukio la kiroho au uchawi. Karla mwanzoni alitumia hirizi na dawa za jadi kabla ya kugeukia sala kama tiba yake.

“Kila siku ninaomba kabla ya kulala ili nisikamatwe tena na wachawi nikiwa usingizini. Inafanya kazi,” anaiambia TRT Afrika. “Ninaomba kwa sababu sitaki nife mikononi mwa mchawi anayenishambulia kwenye ndoto.”

Mtaalamu wa saikolojia kutoka Benin, Kouassi Comlan, ambaye amewatibu wanandoa wengi wanaokumbwa na hali hii, huunganisha mbinu za kisayansi na uelewa wa kitamaduni ili kuwasaidia wagonjwa wake.

“Kupooza usingizini ni ‘parasomnia’ inayotokana na kutengana kwa muda kati ya uamsho wa ubongo na hali ya misuli kushindwa kufanya kazi inayotokea usingizini,” anaeleza Dkt Comlan.

 “Katika hatua hii ya ndoto, ubongo huzima mfumo wa kusogeza misuli ili kuzuia mtu kutekeleza ndoto yake kimatendo. Hali hii inapodumu hata ubongo unapoamka, mtu hupata hisia za kupooza kwa muda, mara nyingi zikiwa na maono au hisia zisizo halisi.”

Uelewa wa kitamaduni wa Dkt Comlan humsaidia kuelewa namna wagonjwa wake wanavyolichukulia jambo hili, akitumia mtazamo jumuishi katika tiba.

“Kama mwanasaikolojia niliyejitahini katika mbinu za kibinadamu na saikolojia chanya, naamini ni muhimu kuliona tatizo hili kwa mtazamo mpana unaojumuisha kipengele cha kifizikia, kiutamaduni, kiroho na maana yake kwa mtu binafsi.”

Hisia za mwili

Dkt Comlan anaeleza kwamba kupooza usingizini hutokea kutokana na kutokulingana kwa mifumo inayodhibiti fahamu na misuli wakati mtu anapobadilika kutoka usingizi hadi pale anpoamka. Kule kushindwa kusogeza misuli kunakoonekana katika usingizi katika hali ya usingizi (Rapid Eye Movement) kunabaki hata ubongo unapokwisha kupata uamsho, hivyo kuunda hali ya mpito isiyo ya kawaida.

Ingawa si hatari kiafya, hali hii inaweza kusababisha msongo mkubwa wa mawazo.

“Kukosa uwezo wa kusogeza mwili mzima hutokea mara nyingi. Mtu anahisi amefungiwa kabisa kimwili, asiweze kuzungumza au kusogea,” anasema.

Kujilinda kiroho

Kama ilivyo kwa Karla, watu wengi wanaopata kupooza usingizini hutafuta msaada kuvunja mzunguko huo. Mila inatoa hirizi na vitendea kazi vya kinga; dini hutoa faraja kupitia sala; na tiba za kisayansi hutoa ufumbuzi wa kiafya.

Mwanachuoni wa Kiislamu kutoka Senegal, Assane Gaye, anaamini kipengele cha kiroho ni muhimu kama mbinu za kisayansi.

“Waumini wengi huliona tukio hili kama nguvu inayojaribu kuathiri au kutisha,” anasema.

“Hata hivyo, Uislamu unafundisha kuwa hakuna linaloweza kumdhuru muumini bila ruhusa ya Allah… ‘Na kama Allah akikuletea madhara, hakuna wa kuyaondoa isipokuwa Yeye’ (Surah Al-An’âm 6:17).”

Anashauri kusoma dua kabla ya kulala, ikiwemo Ayatul Kursiy, akisema humlinda muumini hadi asubuhi.

Kupooza usingizini huchukuliwa tofauti kulingana na tamaduni na imani za mtu.

Wataalamu wanashauri watu kutumia mbinu zozote zinazowasaidia, iwe sala, hirizi, au tiba za kitabibu. Kulala vya kutosha ili kuruhusu akili kupumzika pia husaidia kupunguza hali hii.