Shirika la Umoja wa Mataifa linasema watu wengine 285 wameachwa bila makazi Kordofan Kusini Sudan
Ukosefu wa usalama kumefanya familia kadhaa kukimbia kutoka eneo la Kordofan Kusini
Shirika la Umoja wa Mataifa linalishughulikia wahamiaji lilisema siku ya Alhamisi kuwa watu wasiopungua 285 walikuwa miongoni mwa wale waliondoka katika makazi yao kwenye kipindi cha siku mbili huko mji wa Kadugli na Al-Kuwaik Jimbo la Kordofan Kusini kutokana na hali mbaya ya usalama.
Katika taarifa, Shirika la Kimataifa la Wahamiaji (IOM) linasema maafisa wake wamethibitisha watu 85 wameondoka Kadugli, mji mkuu wa jimbo hilo, kutokana na ukosefu wa usalama na operesheni ya kijeshi Januari 27 na 28.
Shirika hilo limeongexa kuwa watu wengine 200 waliondoka katika makazi yao siku ya Jumatano eneo la mji wa Al-Kuwaik sehemu ya Mashariki huko Kordofan Kusini, pia ikitajwa sababu ya kutokuwa na usalama kama chanzo cha kuondoka kwao.
Kulingana na IOM, familia hizo zilielekea katika jimbo la White Nile kusini mwa Sudan na eneo la Kelik katika jimbo jirani la Kordofan Magharibi.
Shirika hilo limeonya kuwa hali katika eneo hilo bado “ni tete,” likieleza kuwa bado linafuatilia kwa makini yanayoendelea.
Mapema wiki hii, Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na wahamiaji limesema idadi ya walioondoka katika makazi yao eneo la Kordofan imeongezeka hadi 88,316 katika kipindi cha zaidi ya miezi miwili kutokana na vita vinavyoendelea kati ya jeshi na wapiganaji wa Rapid Support Forces (RSF).
Tangu tarehe 15 Aprili, 2023, Jeshi la Sudan na RSF wamekuwa wakikabiliana katika vita ambavyo wapatanishi wa kanda na kimataifa wameshindwa kumaliza. Mapigano hayo yamesababisha vifo vya maelfu ya watu na mamilioni wengine kuondoka katika makazi yao.