Jumla ya viongozi 102 wanaowakilisha nchi 95 na mashirika saba ya kimataifa wanatarajiwa kuhudhuria Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31) nchini Uturuki, huku kukiwa na ushiriki kutoka mabara sita, kulingana na taarifa kutoka Wizara ya Mazingira, Ustawishaji wa Miji na Mabadiliko ya Tabianchi ya Uturuki.
Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, mkutano wa COP31, utakaofanyika Antalya kuanzia tarehe 9 hadi 20 Novemba, utazikutanisha nchi 196 pamoja na Umoja wa Ulaya, ambazo zote ni wadau katika mkataba huo.
Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na wakuu wa nchi 37, wakuu wa serikali 35, makamu wa rais wanane, wana mfalme kutoka nchi mbili , spika mmoja wa bunge, na wawakilishi maalum wanne.
Mashirika saba ya kimataifa pia yamethibitisha kushiriki katika ngazi ya uongozi, nayo ni: Tume ya Ulaya, Umoja wa Mataifa, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Benki ya Dunia, Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), na Shirika la Kimataifa la Nishati (IEA).
Wawakilishi kutoka Afrika
Viongozi na wawakilishi wa ngazi ya juu wanatarajiwa kutoka nchi mbalimbali barani Ulaya, Afrika, Asia, Amerika, na Oceania.
Washiriki kutoka Ulaya ni pamoja na Austria, Uingereza, Bosnia na Herzegovina, Bulgaria, Ufini, utawala wa Wagiriki wa Cyprus, Uholanzi, Uhispania, Uswidi, Italia, Montenegro, Jamhuri ya Kituruki ya Cyprus Kaskazini, Macedonia Kaskazini, Liechtenstein, Malta, Moldova, Norway, Urusi, Slovenia, na Ukraine.
Washiriki kutoka Afrika ni pamoja na Botswana, Burundi, Algeria, Eswatini, Ethiopia, Côte d'Ivoire, Gabon, Guinea-Bissau, Comoro, Jamhuri ya Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Lesotho, Libya, Madagascar, Mali, Mauritania, Msumbiji, Rwanda, Shelisheli, Somalia, Sudan, Tanzania, Togo, na Zimbabwe.
Kutoka Asia na Mashariki ya Kati, washiriki ni pamoja na Azerbaijan, Bangladesh, Falme za Kiarabu, China, Indonesia, Armenia, Palestina, Korea Kusini, Georgia, Iraq, Serikali ya Kikanda ya Wakurdi nchini Iraq, Iran, Qatar, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Kuwait, Lebanon, Maldives, Malaysia, Uzbekistan, Pakistan, Syria, Saudi Arabia, Tajikistan, na Turkmenistan.
Mwitikio ulioratibiwa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi
Mataifa ya Amerika yatawakilishwa na Bolivia, Brazil, Guyana, Venezuela, Antigua na Barbuda, Bahamas, Barbados, Saint Kitts na Nevis, pamoja na Saint Lucia.
Australia, Kiribati, Visiwa vya Marshall, Mikronesia, Niue, Palau, Visiwa vya Solomon, Tonga, na Tuvalu pia vinatarajiwa kushiriki.
Mkutano wa Nchi Wanachama (COP) ndicho chombo cha juu zaidi cha kufanya maamuzi chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), ambao ulipitishwa mwaka 1992.
Nchi zote zilizotia saini mkataba huo zinawakilishwa katika mikutano ya COP, ambapo hupitia utekelezaji wa mkataba huo na nyaraka nyingine za kisheria zinazohusiana nao, kutathmini maendeleo ya kimataifa, na kupitisha maamuzi yanayolenga kuhakikisha mwitikio madhubuti na ulioratibiwa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Maamuzi hupitishwa kwa makubaliano ya pamoja miongoni mwa nchi zote, badala ya kutumia mfumo wa kupiga kura kwa wingi.
Hatua muhimu zilizofikiwa
Jumla ya nchi 196 pamoja na Umoja wa Ulaya (EU) zinawakilishwa katika mchakato wa COP.
Moja ya majukumu makuu ya COP ni kupitia taarifa za kitaifa na orodha za uzalishaji wa gesi zinazosababisha ongezeko la joto duniani, ambazo huwasilishwa na nchi zinazoshiriki.
Kwa miaka mingi, mikutano ya COP imetoa mchango mkubwa katika hatua za kimataifa dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo Itifaki ya Kyoto na Mkataba wa Paris, jambo lililosaidia kuongoza mwelekeo wa sera za kimataifa kuhusu tabianchi.
Katika mkutano wa COP31, Uturuki inashikilia nafasi ya urais wa mkutano huo na ndiyo nchi mwenyeji, huku Australia ikiongoza majadiliano.























