Sokwe wa DRC ajifungua mapacha
Picha zilizotolewa na shirika la habari la hifadhi ya nchi hiyo zilimuonesha sokwe huyo aliyepewa jina la Mafuko mwenye umri wa miaka 22 akiwa amewakumbatia watoto wake.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imeripoti kuzaliwa kwa sokwe mapacha katika Hifadhi yake, na kusema "tukio hilo ni muhimu" kwa sababu wanyama hao adimu wapo hatarini kupotea.
Hifadhi ya Taifa ya Virunga imesema katika taarifa yake kwamba mapacha hao madume waliozaliwa Januari "walionekana wakiwa katika afya njema baada ya uchunguzi."
Sokwe aliyejifungua anajulikana kwa jina la Mafuko.
Hifadhi ya Taifa ya Virunga ina ukubwa wa zaidi ya maili za mraba 3,000, ni Hifadhi kongwe zaidi barani Afrika yenye idadi kubwa ya sokwe wa milimani.
Kutunza mapacha kunaweza kuwa changamoto, "hasa katika miezi ya mwanzo wakati watoto wanategemea matunzo ya mama yao," taarifa ya Hifadhi hiyo ilisema.
Iliongeza kusema kuwa watoto wachanga wanaangaliwa kwa karibu ili kuhakikisha wanakuwa.
Picha zilizotolewa na Shirika la Habari la Hifadhi hiyo zilimuonyesha Mafuko mwenye umri wa miaka 22 akiwa amewakumbatia watoto wake.
Mafuko alizaliwa katika familia ya Kabirizi lakini alijiunga na familia ya Bageni miaka sita baada ya mama yake kuuawa na "watu wenye silaha" mwaka 2007, taarifa ya hifadhi hiyo ilisema.
"Kuzaliwa kwa mapacha hawa kunawakilisha tukio kubwa kwa mienendo ya familia ya Bageni na kwa juhudi zinazoendelea za uhifadhi kusaidia ukuaji wa sokwe wa milimani walio hatarini kutoweka ndani ya Hifadhi ya Kitaifa ya Virunga," ilisema taarifa hiyo.
Kwa jumla, Mafuko sasa amezaa watoto saba, wakiwemo mapacha waliofariki wiki moja baada ya kuzaliwa mwaka 2016.
Familia ya Bageni sasa ina sokwe 59 na ndiyo kubwa zaidi katika hifadhi hiyo, ilisema taarifa hiyo.