Rais wa CAF atembelea Senegal na kutoa wito wa umoja katika soka

Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) Patrice Motsepe amekutana na maafisa wa soka wa Senegal na Rais wa Senegal Bassirou Faye ambapo alitoa wito wa umoja baada ya matukio yaliyojitokeza kufuatia fainali ya AFCON.

By
PICHA YA MAKTABA: Rais wa CAF Patrice Motsepe anasema yuko tayari kwa uchunguzi kuhusu madai ya ufisadi katika Shirikisho hilo. / Reuters

Rais wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) Patrice Motsepe yuko tayari kwa uchunguzi dhidi ya ufisadi kwenye shirikisho hilo, akisema hakuna cha kuficha kufuatia mkutano na maafisa wa Senegal mjini Dakar siku ya Jumatano.

Mwezi uliopita serikali ya Senegal ilitaka kufanyike uchunguzi kuhusu ufisadi baada ya nchi hiyo kupokonywa ubingwa wa AFCON 2025 na Bodi ya Rufaa ya CAF na kombe hilo kupewa wapinzani wao Morocco.

Inafuatia matukio ya vurugu katika mechi ya Januari 18 mjini Rabat ambapo Senegal ilishinda 1-0, lakini kipindi ambacho waliondoka uwanjani kwa dakika kahdaa kupinga maamuzi ya refa.

Motsepe alikutana na maafisa wa Shirikisho la Soka la Senegal na Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye siku ya Jumatano, ambapo alitoa wito wa umoja baada ya matukio ya fainali. Atakuwa nchini Morocco siku ya Alhamisi kwa mikutano kama hiyo.

‘Kukabiliana na ufisadi’

“Niko tayari kwa uchunguzi kuhusu ufisadi CAF, uwe unafanywa na serikali au taasisi nyingine yoyote ile,” Motsepe aliwaambia waandishi wa habari. “Hakika, ningependekeza hilo lifanyike. Tutatoa ushirikiano kikamilifu.

“Niliwaambia kumewahi kuwa na matatizo na tukaingilia kati. Siyo tu katika soka, lakini pia katika biashara na siasa. Hatuwezi kuwaonesha watoto wetu mtazamo kwamba ukitaka kufanikiwa maishani, uwe mfisadi. Lazima tukabiliane na ufisadi kabisa.

Motsepe hakutaka kuzungumzia suala la Senegal na Morocco ambalo kwa sasa liko katika Mahakama ya Upatanishi ya Michezo.

Upendeleo

“Siwezi kuwaambia jambo ambalo sijawahi kuzungumzia hapo awali mara 10, 15, 20. Unaweza kuniuliza swali hilo hilo mara 100, nitakujibu hivyo hivyo mara 100. Ni wajibu wangu kuheshimu kwamba suala hilo liko mbele ya mahakama ya juu ya michezo duniani.”

Motsepe alipinga wazo lolote kuwa Morocco imependelewa katika mchakato wa kukata rufaa.

“Haiwezekani kwa nchi yoyote barani Afrika kupendelewa zaidi ya nyingine. Hilo halitofanyika,” alisema.

“Tuna imani tutapita katika changamoto hizi na kuibuka tukiwa kitu kimoja mataifa 54 ya bara Afrika.”