| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Mwendesha Mashtala wa ICC asimamishwa kazi kwa madai ya dhulma za ngono
Karim Khan atafikishwa kwa kamati ya nidhamu ambayo inawakilishwa na mataifa wanachama 125, kulingana na ICC.
Mwendesha Mashtala wa ICC asimamishwa kazi kwa madai ya dhulma za ngono
Picha: Mahmoud Hjaj / AA

Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya ICC Karim Khan amesimamishwa kazi kuanzia Jumatatu kufuatia uchunguzi wa madai ya dhulma za ngono.

ICC ilitangaza uamuzi huo, ikisema Khan atafikishwa kwa kamati ya nidhamu ambayo inawakilishwa na mataifa wanachama 125 kufuatia matokeo ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa, ambao haujawekwa wazi kwa umma.

"Tathmini ya ICC ni kulingana na ripoti ya uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa (OIOS), ushahidi uliopo, ushauri wa kamati ya wataalamu wa sheria, na ushahidi wa maandishi," ICC ilisema katika taarifa.

"Uamuzi wa ICC na nyaraka zingine utabaki kuwa siri. Mahakama imetoa wito wa kuheshimiwa kwa faragha na haki za pande zote zinazohusika, pamoja na kuzingatia mchakato unaoendelea," iliongeza.

Mkutano mkuu utalishughulikia suala hilo "mara moja."

Khan, ambaye alienda likizo Mei 2025 wakati uchunguzi wa Umoja wa Mataifa ukiendelea , alisema mwezi Aprili kuwa “ameondolewa lawama.”

Khan aliliambia shirika la habari la Zeteo katika mahojiano kuwa uchunguzi huo hawakumpata “na makosa ya dhulma za ngono au matumizi mabaya ya mamlaka” na kwamba anatakiwa kuruhusiwa kurudi kazini.

“Nimeisoma ripoti ya Umoja wa Mataifa. Nimesoma matokeo ya uchunguzi wa majaji. Na katika ripoti ya Umoja wa Mataifa, kuna ripoti za uchunguzi 137. Hakuna hata moja ambayo inaonesha makosa kwa njia yoyote ile ,” alisema.

Mwezi Machi, jopo la majaji watatu lilikubaliana kwa pamoja kuwa matokeo ya uchunguzi wa Umoja wa Mataifa “hayana msingi wa makosa au ukiukwaji wa majukumu kwa mujibu wa sheria zilizopo,” kulingana na shirika la Middle East Eye.

Uchunguzi huo ulianzishwa na Mkuu wa Baraza la ICC, mwezi Novemba 2024 baada ya mfanyakazi katika ofisi ya Khan kumshtumu kwa madai ya dhulma za ngono.

Mwezi Agosti, mwaka uliopita mwanamke wa pili alijitokeza, akidai mwendesha mashtaka alitumia vibaya mamlaka yake wakati akifanya kazi katika ofisi yake.

Madai hayo yanakuja huku ofisi ya Khan ikifuatilia madai ya uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki ya maafisa wa Israel na wanajeshi huko Gaza na maeneo ya Palestina yanayokaliwa.

Mwezi Mei 2024, Khan alitangaza kuwa atatoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wake wa ulinzi wakati huo, Yoav Gallant, kuhusiana na "uhalifu" kwa madai ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu Gaza.

CHANZO:AA