| Swahili
AFRIKA
1 dk kusoma
Wabunge watoro Tanzania, wapewa siku nne na Spika kujieleza
Spika Zungu pia amewaonya wabunge ambao wameonesha tabia ya utoro bunge na kuwataka waache mara moja tabia hiyo kabla hawajachukuliwa hatua za kinidhamu.
Wabunge watoro Tanzania, wapewa siku nne na Spika kujieleza
Spika wa Bunge la Tanzania amewataka wabunge watoro kuacha tabia hiyo. / TRT Afrika Swahili

Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Hassan Zungu, amesema wabunge waliokwenda nchini Morocco kushuhudia mchezo wa Tanzania dhidi ya Senegal hawakutoa taarifa rasmi wala kuaga, hivyo wanatakiwa kujieleza kwa Katibu wa Bunge ndani ya siku nne.

Akizungumza bungeni, Spika Zungu alisema hatua hiyo inalenga kulinda uwajibikaji na utaratibu wa viongozi wa umma, hasa pale wanaposafiri nje ya nchi bila kufuata kanuni na taratibu za kibunge.

Kauli hiyo imekuja baada ya baadhi ya wabunge kuonekana nchini Morocco wakishuhudia mchezo wa hatua ya mtoano wa michuano ya Afrika kati ya Tanzania na Senegal.

Katika mchezo huo wa kusisimua, Tanzania iliondolewa kwenye mashindano kwa mikwaju ya penalti baada ya kutoka sare katika muda wa kawaida wa mchezo, hali iliyomaliza safari ya Tanzania kwenye mashindano hayo.

Spika Zungu alisema Katibu wa Bunge atawapa wabunge hao siku nne kutoa maelezo rasmi kuhusu safari yao na sababu za kutofuata utaratibu wa kuaga kabla ya kuondoka nchini.

Wakati huo huo, Spika Zungu pia amewaonya wabunge ambao wameonesha tabia ya utoro bunge na kuwataka waache mara moja tabia hiyo kabla hawajachukuliwa hatua za kinidhamu.