Donald Trump ametishia kumfunga mwanahabari aliyetoa taarifa kuhusu uokoaji wa rubani Iran

Donald Trump anasema mwanahabari atakayekataa kufichua vyanzo vya ripoti kuhusu uokoaji wa rubani wa Marekani nchini Iran atafungwa jela.

By
Trump aweka shinikizo dhidi ya vyombo vya habari kuhusu anachikitaja kuwa hatari kwa 'usalama wa taifa'. / AP

Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema mwanahabari aliyeripoti kwanza kuhusu kuokolewa kwa rubani wa Marekani nchini Iran afichue chanzo cha taarifa hizo, au afungwe jela.

Trump pia amelalamika faraghani kwa wasaidizi wake kuwa namna vyombo vya habari vinavyoripoti kuhusu vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran imekuwa hasi sana.

Baada ya ndege ya kivita ya Marekani kudunguliwa na kuanguka nchini Iran siku ya Ijumaa, vyombo kadhaa vya habari viliripoti kuwa mmoja wa marubani wawili aliyekuwa ndani ya ndege hiyo aliokolewa kwa mafanikio.

Trump amesema kuwa kufichuliwa kwa taarifa hiyo kulihatarisha usalama wa operesheni inayoendelea ya kumuokoa rubani wa pili, ingawa hatimaye naye aliokolewa.

"Hatukutoa taarifa kuhusu uokoaji wa kwanza kwa saa limoja. Kisha kuna mtu akatoa taarifa hio, natumaini tutampata aliyetoa hio taarifa. Tunajitahidi sana kumtafuta skumpata aliyevujisha taarifa hiyo," Trump alisema.

Tishio kwa vyombo vya habari

“Tutakwenda kwa kampuni ya habari iliyochapisha taarifa hiyo, na tutasema, ‘Usalama wa taifa — toeni taarifa hizo au mtaenda jela.’”

Haikuwa wazi ni chombo gani cha habari au mwanahabari gani Trump alikuwa akimlenga.

Vyombo kadhaa, ikiwemo The New York Times, CBS News, na Axios, viliripoti kuhusu operesheni hiyo ya uokoaji.

Mwenyekiti wa Mawasiliano nchini Marekani, Brendan Carr, ameandika kwenye mtandao wa kijamiii wa X kwamba vituo vya utangazaji vinavyotoa “habari za uongo” vina nafasi ya “kurekebisha mwenendo wao kabla ya leseni zao kufanyiwa upya.”

Hii ilifuatia ujumbe wa Trump uliodai kuwa “Magazeti na vyombo vya habari vya kiwango cha chini vinataka tushindwe katika vita.”