Jose Mourinho: Kocha mahiri ''The Special One''

‘The Special One’ ni mmoja tu duniani. Huyu si mwingine, ni Jose Mourinho.

By
Meneja Jose Mourinho. / Reuters

Unajua kuwa ‘The Special One’ alishawahi kusukuma gozi katika ligi za pale Ureno, akichezea nafasi ya kiungo, kabla ya kutundika daluga akiwa na umri wa miaka 24 tu?

José Mário dos Santos Mourinho Félix, huyu huyu, ambaye aliwahi kula bata pale kwenye fukwe za Diani kusini mwa pwani ya Kenya akiwa na familia yake mwaka 2010, ni kati ya mameneja wenye mafanikio makubwa duniani, akishinda ubingwa katika mataifa manne.

Mourinho alijipa hadhi ya ‘The Special One’ kwenye mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari katika utambulisho wake mwaka 2004, akiwa tu, ametokea kuwapa taji la Mabingwa Ulaya (UEFA), baada ya kuiongoza Porto ya Ureno kwenye ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Monaco ya Ufaransa.

Kwa sasa, yeye ndiye meneja wa Benfica ya Ureno, timu ile ile, iliyotia shubiri kwenye sukari ya Real Madrid ya Hispania, kwa kuidhalilisha kwa mabao 4-2, kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa barani Ulaya.

Majukumu yake ya kwanza pale Sporting CP na Porto alikuwa mkalimani wa kocha Muingereza Bobby Robson kabla ya kuwa kocha msaidizi pale Barcelona.

Kisha akawa meneja wa Benfica na kurudi Porto ambako aliwasaidia kunyanyua ndoo ya Ligi kuu mara mbili.

Mwaka 2004 akatua Stamford Bridge, Magharibi mwa jiji la London. Hapo ‘The Special One’ alifanya ya kwake, kufikia kipindi anaondoka mwaka 2007 Mourinho alikuwa ameshinda mataji mawili ya Ligi Kuu, Kombe la FA, na mataji mawili ya Kombe la ligi.

2008 akasogea Italia akiwa na Inter Milan, msimu wake wa kwanza tu wakawa mabingwa wa Ligi ya Serie A. Mwaka 2010 akashinda mataji matatu tofauti ikiwa ni mara ya kwanza kwa klabu ya Italia kupata ushindi huo katika historia.

Mourinho, ambaye aliweka wazi kuwa huwa haangalii mtindo wa uchezaji, bali yeye hujali matokeo tu, aliwahi kuchaguliwa kuwa kocha bora wa mwaka wa FIFA.

Msimu wa 2011-2012 akatwaa ubingwa wa La Liga akiwa na Real Madrid, ya akina Cristiano Ronaldo, Sergio Ramos, Kaka na Iker Casillas Fernández, akawa kocha wa tano kushinda Ligi Kuu katika nchi nne tofauti.

Ama kwa hakika, ni kipindi cha Mourinho pale nchini Hispania, ndiko kuliko pandisha hadhi na joto za mechi za El Classico, kati ya Real Madrid na Barcelona.

Si unakumbuka zile vurugu za akina Sergio Ramos na Gerard Piqué?

Mwaka 2013, ‘The Special One’, akarejea tena darajani, na kuwarudishia tabasamu matajiri hao wa zamani wa jiji la London, akiwapa Ligi Kuu ya England na Kombe la Ligi.

Meneja huyo mwenye umri wa miaka 63 pia amezinoa timu za Manchester United na Tottenham Hotspur.

Aliwahi kuwa pale Roma, Italia na kuifua timu ya Ligi Kuu ya Uturuki Fenerbahce. Alitimuliwa na klabu hiyo ya Istanbul 2025 baada ya kushindwa kufuzu kwa ligi ya mabingwa Ulaya.

Katika hatua ya mtoano ligi ya mabingwa Ulaya Benfica itakutana tena na Real Madrid, je, ‘The Special One’ ataweza kuuangusha tena mbuyu katika mikondo miwili?