| Swahili
AFRIKA
2 dk kusoma
Afrika Kusini yamkamata mwanaharakati wa Benin Kemi Seba kwa tuhuma za uchochezi
Kemi Seba na mwanawe walikamatwa mjini Pretoria pamoja na mtu mwingine ambaye anadaiwa kuwasaidia kuingia Zimbabwe kwa njia haramu kwa malipo, polisi imesema.
Afrika Kusini yamkamata mwanaharakati wa Benin Kemi Seba kwa tuhuma za uchochezi
Benin ilitoa hati ya kimataifa ya kumkamata Disemba 2025. / Reuters
tokea masaa 4

Polisi Afrika Kusini imesema kuwa imemkamata mwanaharakati Kemi Seba siku ya Alhamisi, ambae alikuwa anatafutwa nchini Benin kwa tuhuma za "kuchochea uasi" baada ya kuunga mkono mapinduzi ya Disemba yaliyofeli.

Seba, ambae jina lake kamili ni Stellio Gilles Robert Capo Chichi, mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Pan-Africanist Emergency pia anajulikana kwa maneno makali dhidi ya Ufaransa na serikali za Afrika zinazoshirikiana na Ufaransa.

Alikamatwa mjini Pretoria Jumatatu akiwa pamoja na mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 18, pamoja na mtu mwengine anayetuhumiwa kwa kuwaingiza katika nchi jirani ya Zimbabwe kinyume cha sheria kwa malipo

Walikuwa wanaelekea Ulaya.

"Uchunguzi wa awali umeonesha kuwa Seba alikuwa anatafutwa na Ufaransa na Benin kwa uhalifu dhidi ya serikali," imesema taarifa.

Kesi yake imeahirishwa hadi Aprili 20 na Seba na mtoto wake watabaki chini ya uangalizi wa polisi huku mchakato wa kuwarudisha Benin ukiendelea, imesema taarifa hiyo.

Hati ya kimataifa ya kumkamata

Benin ilitoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa Seba Disemba 12 baada ya kuunga mkono mapinduzi yaliyofeli ambapo wanajeshi walidai kupitia televisheni kwamba wamempindua Rais Patrice Talon.

Jaribio la kupindua serikali Disemba 7 lilidhibitiwa ndani ya saa kadhaa kwa usaidizi wa jeshi kutoka Nigeria na Ufaransa.

Seba, ambae amemtuhumu Talon kwa kuwa karibu na koloni la Ufaransa, aliweka video akitangaza "siku ya ukombozi" kwa nchi yake.

Hati ya kukamatwa ilikuwa ni uthibitisho wa makosa yake dhidi ya usalama wa nchi na kuchochea uhalifu," imesema Serikali ya Benin.

Nchi hiyo ya Afrika Magharibi imewakamata takriban watu 30 baada ya jaribio la mapinduzi, wengi wao wanajeshi, vyanzo vya kisheria vimeiambia AFP, huku wengi wa waasi wakikimbia.

Seba alizaliwa Ufaransa na wazazi kutoka Benin, ameshtakiwa Ufaransa mara kadhaa. Alipokonywa uraia wa Ufaransa mwaka 2024.