Kwa siku ya pili mfululizo tangu kuanza tena kwa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Iran, Marekani imeshambulia daraja muhimu la reli kaskazini mwa Iran linalounganisha nchi hiyo na China pamoja na Urusi, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars la Iran.
Shirika hilo limesema shambulio hilo la kombora la masafa marefu limelenga daraja la reli la Ogtay Khan lililoko katika mkoa wa Golestan, kaskazini mashariki mwa Iran, mapema Alhamisi.
Shambulio hilo limeripotiwa kutokea wakati Iran ilipositisha huduma za treni kwa abiria kati ya Tehran na mji wa Mashhad ulioko kaskazini mashariki mwa nchi, kufuatia kile ambacho wakazi wa eneo hilo walidai kuwa ni shambulio la pamoja la Marekani na Israel lililoharibu sehemu ya njia hiyo ya reli.
Iran ilisema wafanyakazi wametumwa kufanya ukarabati walitumwa katika eneo hilo na kwamba abiria waliokwama watasafirishwa kwa barabara hadi Mashhad.
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imesema imetekeleza mashambulizi zaidi dhidi ya Iran ili kudhoofisha uwezo wa Iran wa kutishia uhuru wa usafiri baharini katika Mlango-Bahari wa Hormuz.
Iran na Marekani mnamo Juni 17 zimefikia makubaliano yaliosimamiwa na Pakistan yenye lengo la kumaliza mzozo wao wa kijeshi na kuandaa njia ya makubaliano ya amani ya kudumu.
Hata hivyo, siku ya Jumatano, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kwamba makubaliano hayo "yameisha," na hivyo kusababisha duru mpya ya makabiliano ya kijeshi.











