Wengi wanamfahamu kwa jumbe zake zneye utata kwenye mitandao ya kijamii, hasa ule wa X.
Huyu si mwingine, bali ni Jenerali Muhoozi Kainerugaba, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, na mtoto wa kiongozi wa nchi hiyo, Yoweri Kaguta Museveni.
The ‘Tweeting General’, kama anavyofahamika, amepanda vyeo vya kijeshi kwa muda mfupi sana hadi kufikia kuwa na nyota nne.
Unafahamu kuwa Muhoozi amezaliwa jijini Dar es Salaam nchini Tanzania miaka 51 iliyopita?
Jenerali huyu amekuwa sauti na sura ya jeshi la nchi hiyo kwa muda mrefu.
Aliwahi kuonesha nia ya kugombea urais wa Uganda, kabla ya kubadili ‘gia angani’ na kuamua kumuunga mkono baba yake.
Tukisogea Rwanda, tunakutana na Kapteni Ian Kagame na Luteni Brian Kagame, japo anayefahamika zaidi hapa ni Ian Kagame.
Ian, ambaye amezaliwa miaka 30 iliyopita, ni sehemu ya timu ya ulinzi wa rais wa nchi hiyo, Paul Kagame.
Akiwa sehemu ya jeshi la RDF la nchini Rwanda, Ian Kagame anawajibika kuhakikisha usalama wa kiongozi wa nchi hiyo, kwa wakati wote, haswa anapokuwa kwenye hadhara.
Kama ilivyo kwa Muhoozi, Ian Kagame pia alipata mafunzo ya kijeshi kutoka Royal Military Academy Sandhurst cha nchini Uingereza.
Kusini mwa Afrika yupo Meja Sean Mnangagwa, mtoto wa rais wa taifa hilo, Emmerson Mnangagwa.
Afisa huyu wa jeshi ni sehemu ya kikosi cha ulinzi wa watu maarufu nchini humo.
Alipata mafunzo yake ya kijeshi katika nchi mbalimbali, zikiwemo Zimbabwe, China, Urusi na Msumbiji.
Wakati fulani, afisa huyu wa jeshi aliwahi kuibua ‘sintofahamu’ nchini humo, baada ya kubainika kuwa amejichora tattoo mkononi, wengi wakihoji kanuni za jeshi la nchi hiyo kuhusu wanajeshi kujichora miili yao.



















