Jeshi la Sudan limetangaza kupelekwa kwa wanajeshi zaidi kutoka kwa vikosi washirika katika jimbo la Blue Nile, huku shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu uhamiaji likisema watu 730 waliondolewa katika vijiji vitano Kusini kwa Kordofan kutokana na hali mbaya ya usalama.
Katika taarifa siku ya Jumanne, jeshi lilisema Meja Jenerali Ismail al-Tayeb, kamanda wa kikosi cha 4, alivipokea vikosi hivyo vya pamoja, ambavyo vilishirikiana katika operesheni dhidi ya Rapid Support Forces (RSF) katika jimbo la kusini mashariki la Blue Nile nchini Sudan.
Tayeb anasema vikosi hivyo vilikuwa tayari kuendelea na operesheni, akiongeza kuwa RSF na washirika wake “walikuwa wamezidiwa kimashambulizi”.
Kuongezeka kwa mashambulizi
Kumekuwa na mapigano zaidi katika jimbo la Blue Nile kwenye kipindi cha siku mbili zilizopita baada ya mashambulizi ya RSF maeneo kadhaa kwenye jimbo hilo.
Siku ya Jumamosi, jeshi la Sudan lilitangaza kuwa linatuma kikosi kingine kutoka kwa idara ya ujasusi kuimarisha operesheni za kijeshi eneo la Bukkori jimbo la Blue Nile.

























