Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe ameonesha wasiwasi wake kufuatia operesheni zilizoendeshwa na jeshi la DRC za kuwapokonya silaha wapiganaji wa Jeshi la Kidemokrasia la Ukombozi wa Rwanda walioko DRC.
Uwepo wa wanajeshi wa FDLR nchini DRC, ni moja ya mambo yaliyoangaziwa katika mkataba wa amani wa Washington, uliosainiwa mwaka jana.
Akizungumza katika gwaride maalumu lililofanyika Kisangani siku ya Jumapili, Naibu Kamanda wa Majeshi ya DRC, Jenerali Jacques Ychaligonza aliwataka wapiganaji wa FDLR wasalimishe silaha zao kwa hiyari, ili kuepuka vifo zaidi katika eneo hilo.
Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya maofisa wa DRC na Rwanda kukutana jijini Washington Machi 17 na 18 mwaka huu, kujadiliana namna ya utekelezwaji wa mkataba wa amani wa Washington.
Hata hivyo, kwa upande wake, Nduhungirehe alisema yupo tayari kuona utekelezaji wa vitendo na sio ahadi tu.










