Cape Verde, Mauritius na Ushelisheli wafanikiwa kuangamiza surua na rubela
WHO imetangaza kuangamizwa kwa magonjwa ya Surua na Rubela nchini Mauritius, Ushelisheli na Cape Verde, ikiwa ni mara ya kwanza kwa mafanikio hayo kusini mwa jangwa la Sahara.
Katika mafanikio makubwa ya afya ya umma, Cabo Verde, Mauritius na Seychelles zimeondoa surua na rubela, na kuwa nchi za kwanza kusini mwa Jangwa la Sahara kufikia hatua hii.
Tume ya Shirika la Afya ya kukabiliana na maradhi hayo ilitangaza mafanikio hayo Jumatatu likipongeza kama hatua kubwa kwa Afrika.
Naibu waziri wa Afya nchini Mauritius Anishta Babooram alisema kuwa hii matokeo ya kujitolea kwa taasisi za afya nchini humo lakini mtihani mkubwa ni kuhakikisha hautokei tena maambukizi kutoka nje.
"Kuondoa sio mwisho wa safari. Kudumisha hadhi hii kunahitaji umakini wa mara kwa mara, ugunduzi wa haraka na majibu ya haraka kwa maambukizi yoyote kutoka nje,’’ alisema Waziri Babooram. ‘‘Mauritius inasalia kujitolea kikamilifu kudumisha chanjo ya juu, kuimarisha usalama wa afya kuvuka mpaka na kuimarisha mifumo ya tahadhari ya mapema," aliongeza.
Utoaji chanjo
Nchini Mauritius, hakuna maambukizi ya surua ambavyo vimeripotiwa tangu 2019. Nchi ilijibu mlipuko wa surua wa 2018-2019 kwa juhudi mpya za chanjo na uchunguzi. Kufikia 2024, chanjo ya surua,matumbwitumbwi na rubela katika ngazi ya kitaifa ilifikia 98% kwa kipimo cha kwanza na 96% kwa kipimo cha pili.
Ushelisheli imedumisha chanjo ya zaidi ya 95% kwa dozi ya kwanza na ya pili ya chanjo ya surua kwa zaidi ya miongo miwili, ikisaidiwa na ufuatiliaji wa makini, uthibitisho wa kimaabara na uchunguzi wa afya katika maeneo ya kuingia.
Mlipuko wa mwisho wa surua ulidhibitiwa mnamo 2020. Hakuna kesi ya rubela iliyothibitishwa tangu 2016.
"Juhudi hizi endelevu zimekuwa na changamoto lakini kupitia kwa kujitolea kwa Programu yetu ya upanuzi ya timu ya chanjo tumefanikiwa kuzuia maambukizi ya surua na rubela kwa miongo kadhaa," alisema Marvin Fanny, Waziri wa Afya wa Ushelisheli. "Ninajivunia kutangaza kwamba, Ushelisheli imetangazwa kama isiyo na surua na rubela, mafanikio makubwa kwa taifa letu."
Kuzuia vifo
Nchi nyingine Afrika iliyotangazwa pia kuangamiza Surua na Rubela ni Cape Verde ya Magharibi mwa Afrika.
Tangu mwaka wa 2001, nchi nyingi katika kanda ya Afrika zimetekeleza mikakati ya kudhibiti surua ambayo ni pamoja na kutoa dozi mbili za msingi za chanjo, kufanya kampeni za mara kwa mara za chanjo nyingi, ufuatiliaji wa kina wa magonjwa na uboreshaji wa mwitikio wa milipuko pamoja na utunzaji wa kimatibabu kwa wagonjwa wa surua.
Kati ya 2000 na 2023, juhudi hizi zinakadiriwa kuzuia karibu vifo milioni 21, punguzo la 79% la vifo vinavyokadiriwa kila mwaka katika kipindi hiki.
Kwa miaka mingi, utoaji wa chanjo barani Afrika umeongezeka. Mnamo 2024, chanjo ya dozi ya kwanza ya chanjo ya surua na rubela ilifikia 71%, kutoka 67% mnamo 2022, wakati chanjo ya kipimo cha pili ilipanda kutoka 43% hadi 55% katika kipindi hicho.